Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa amepongeza jitihada zinazofanywa na
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuweka mazingira wezeshi ya
kuendesha shughuli za sanaa na michezo nchini kwa kuchukua hatua
mbalimbali za kimkakati ambazo zimeanza kuzaa matunda katika kipindi
kifupi.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya Februari 12, 2022 kwenye
dhukuru na wadau wa tasnia ya Filamu iliyofanyika jijini Dar es Salaam
ambapo amesisitiza kuwa dhamira yake pia ni kuona sekta ninazozisimamia
zinapiga hatua kubwa za kimaendeleo, na kuleta mapinduzi makubwa ambayo
hayajawai kutokea. Ametaja baadhi ya mazingira wezeshi ambayo Mhe. Samia
ameyaweka katika kipindi hiki kuwa ni pamoja na kuandaa filamu ya Royal
Tour inayolenga kuitangaza Tanzania katika Nyanja mbalimbali za
uwekezaji ikiwemo katika sekta ya filamu ambayo yeye mwenyewe ameshiriki
kikamifu katika filamu hiyo.
Pia amesema Mhe. Rais ameridhia
kutenga fedha za maendeleo ya sanaa na michezo, kiasi cha Shilingi
Bilioni 2.5 kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni ambazo
zitawasaidia wasanii kupewa mikopo midogo midogo kwa ajili ya kuandaa
kazi zao na kuzirejesha taratibu na bila riba.
Amesema katika
kipindi hiki bajeti ya Wizara yake imeongezeka ili kuiwezesha
kukamilisha programu zake za maendeleo na kufikia malengo yake
iliyojiwekea, ikiwemo utafutaji masoko ya filamu zinazozalishwa nchini.
Amefafanua
kwamba Wizara tayari imeimarisha mifumo ya urejeshwaji wa faida ya kazi
za sanaa kupitia mirabaha, ambapo sekta ya filamu ni miongoni mwa sekta
zilizoanza kunufaika.
Pia kuimarisha uhusiano wa kimataifa ili
kufungua milango nje ya nchi na kutoa fursa kwa bidhaa za kitanzania
hususan filamu kuuzika katika soko la kimataifa.
Kwa upande
mwingine amesema Serikali inakwenda kuanzisha programu ya kuzalisha
filamu kubwa za kitaifa zitakazokuwa zinafadhiliwa na Serikali mahususi
kwa ajili ya kuhifadhi historia, utamaduni, pamoja na kutangaza nchi na
kuongeza viwango vya ubora wa filamu zinazozalishwa nchini.
Kununua
na Kuanzisha maktaba ya vifaa vya filamu vya kisasa itakayotoa fursa
kwa wadau kupata vifaa bora na kwa gharama nafuu ili kuboresha filamu
zinazoandaliwa nchini.
Kuhusu kilio cha muda mrefu cha waandaji
wa filamu Mhe Mchengerwa amesema Wizara inakwenda kuandaa mwongozo kwa
wanunuzi wa filamu hapa nchini kununua filamu hizo kwa bei
inayomfaidisha mwandaaji wa filamu hiyo pamoja na wasanii kiujumla.
Amesema
Serikali itajenga jijini dodoma jengo la kisasa ikiwa ni kitega uchumi
kwa ajili ya kuwezesha mfuko wa sanii na kutoa huduma za pamoja (One
Stop Service Centre) pia nyumba zenye hadhi na kwa gharama nafuu wasanii
ili kulinda heshima na hadhi ya wasanii.
Naye Katibu Mkuu Dkt.
Hassani Abbasi amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuongoza kikao hicho kwa
mafanikio makubwa huku akifafanua kuwa kila upande unamambo ya
kuyatekeleza ambapo kwa upande wa Wizara amemwagiza Mkurugenzi wa Sanaa
kuyaainisha yote na kuyapatia ufiumbuzi mara moja.
Awali Mtendaji
Mkuu wa Bodi ya Filamu nchini Kiagho Kilonzo amesema tasnia ya filamu
imekuwa ikikua kila kukicha hivyo ushirikiano wa wadau wote ni muhimu
kufikia mapinduzi ya kweli ya filamu nchini. Wakichangia kwa nyakati
tofauti wadau hao wamempongeza Waziri Mchengerwa kwa ubunifu wa kuwa na
dhukuru na wadau ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao kwa
pamoja.