ADC kulea watoto, kufuta madeni wadaiwa Bodi ya Mikopo

MGOMBEA Urais kupitia tiketi ya chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Wilson Mulumbe amesema endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi ataondoa makato ya mikopo ya vyuo vya Elimu ya Juu inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, pamoja na kutoa umeme bure kwa wananchi.

Aidha Mulumbe amesema ataweka mfuko wa kumsaidia mtoto tokea anazaliwa hadi anapofikisha miaka 18, pamoja na wananchi kuunganishiwa umeme bure katika maeneo mbalimbali hapa nchini, yakiwamo maji.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi, Mulumbe ambaye aliambatana na mgombea mwenza Shoka Khamis Juma, amesema miezi mitatu mara baada ya kuapishwa atayafuta madeni ya wahitimu wa vyuo vikuu yote.

Aidha amesema ndani ya miezi hiyo pia wananchi wote wanakwenda kuunganishiwa umeme bure katika maeneo mbalimbali, lengo ni kutaka wananchi wanaotumia umeme wafikie asilimia 100.

"ADC tunataka tutoke kwenye asilimia 37 za matumizi ya umeme hadi kufikia asilimia 100 na hili linawezekana na tumejipanga kwenye haul,"amesema Mulumbe.

Kuhusu mfuko wa kulea watoto mara tu wanapozaliwa amesema mfuko huo utakuwa ukitumika kulea mtoto tangu anazaliwa hadi anapofika miaka 18, ndipo wazazi wataendelea kumlea wao wenyewe.

Amesema ADC imeamua kuondoa mikopo hiyo kwa sababu watu hao ni tegemezi kwa taifa na ni wataalamu ambao taifa linahitaji kuwatumia katika maeneo mbalimbali, kwa ajili ya kuleta maendeleo.

"Nikiapishwa ndani ya miezi mitatu nakwenda kufuta madeni ya wahitimu wa vyuo vikuu ambayo wanadaiwa kutokana na mikopo waliyopewa wakiwa vyuoni," amesema Mulumbe.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii