Polisi nchini Uganda
wanamshikilia mwanaume mmoja baada ya kukutwa na bomu la mkononi aina ya “guruneti”
(Grenade) wakati wa uchaguzi wa awali wa chama tawala cha NRM .
Kwa mujibu wa NTV
Uganda, tukio hilo limetokea eneo la Kamubezi lililopo Isingiro Kusini nchini humo,
ambako taratibu za uchaguzi wa ndani wa chama hicho tawala kinachoongozwa na
rais Yoweri Museven ulikuwa ukiendelea mapema leo hii.
Inadaiwa kuwa, mwanaume
huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi mpaka hivi sasa, ni miongoni wa wafuasi
wa kambi ya mtia nia wa nafasi ya ubunge katika chama hicho anayefahamika kwa
jina la Maari Mujuni, na alikuwa na dhumuni la kuvuruga zoezi hilo ambalo
linawahusisha watia nia wengine ambao ni Alex Bakunda, Gilbert Rwabambari na
Rudoviko Byarugaba
Aidha katika uchaguzi
huo ambao unalenga kuwapata wagombea mbali mbali watakaopeperusha bendera ya
chama cha NRM (National Resistance Movement) katika Uchaguzi mkuu ujao, kumeripotiwa matukio mbali mbali
yanayohusisha vurugu katika maeneo tofauti, huku vyombo vya usalama vikitoa
onyo kali kwa watakaovuruga amani kupitia zoezi hilo