MAONESHO ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea yakitoa fursa kwa washiriki kuonesha bidhaa zao, huduma na teknolojia kwa lengo la kufi kia masoko mapya na kutafuta fursa mpya.
Sambamba na bidhaa mbalimbali, ni kawaida katika maonesho hayo kushuhudia kazi za kibunifu na uvumbuzi wa ama watu binafsi au taasisi za Kitanzania ikiwa ni hatua muhimu ya kuhamasisha maendeleo kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
Mfano, katika gazeti hili leo ipo taarifa kuhusu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Hisabati, kwamba wamebuni mfumo wa kusaidia wanafunzi kujifunza Hisabati bila mwalimu, ambao umeonesha matokeo chanya kwa wanafunzi.
Vilevile, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetengeneza mifumo ya akili mnemba itakayomsaidia mtu binafsi na daktari kupima afya ya akili kwa mtu mwenye msongo wa mawazo kutokana na changamoto mbalimbali.
Aidha, Udom imeboresha utengenezaji wa roketi itakayotumika kusafirisha vifaa kwenda angani vitakavyosaidia kutengeneza mvua katika kipindi ambacho zitakata na maeneo ambayo hayapati mvua ya kutosha.
Kazi hizo za kibunifu, zinatoa changamoto kwa mamlaka na wadau kuzichukulia kwa uzito na kuhamasisha mchakato wa kuziendeleza ili zilete tija kwa taifa na watu wake kwa ujumla.
Kwa hiyo, uvumbuzi wa namna hii haupaswi kuishia kwenye maonesho bila kusikia wala kuona uendelevu wake
kwa maana ya kufikia kiwango cha matumizi ya kila siku au masoko makubwa.
Kutokuwapo mikakati ya kufuatilia na kuendeleza ubunifu na wabunifu hawa, ni hasara kubwa kwa taifa kwani inakwamisha mafanikio ya teknolojia na ubunifu unaoweza kuboresha maisha ya wananchi na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.
Ili kuhakikisha uvumbuzi unafaidisha umma, mamlaka zinapaswa kuanzisha na kuimarisha mifumo madhubuti ya kuendeleza uvumbuzi huo kutoka hatua ya awali hadi utekelezaji ili utumike kwa manufaa ya wengi.
Tunahimiza kuwapo ushirikiano madhubuti kati ya wavumbuzi na wabunifu na serikali ili kuharakisha, kuhalalisha na kuendeleza teknolojia zinazoweza kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi kama hizi ambazo zimewasilishwa kwenye maonesho.
Ni matumaini yetu kwamba kazi za ubunifu na uvumbuzi wa namna hii hazitaishia kwenye maonesho bali zitafanyiwa mchakato unaostahili kuzihalalisha zitumike moja kwa moja, ziwe wazi kwa ajili ya kutumiwa na yeyote.
Kwa kufanya hivyo, itawezekana kuleta molari kwa wabunifu na wavumbuzi kuendeleza teknolojia zinazobeba suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi, na kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa katika nyanja mbalimbali.