Shigongo Azindua Kivuko Cha MV Mwanza, Aishukuru Serikali kwa Kuimarisha Usafiri Buchosa

KIVUKO kipya cha MV Mwanza Julai 2, 2025 kimepokelewa kwa shangwe kubwa katika Jimbo la Buchosa mnamo Julai 2, 2025, ambapo kitahudumu kati ya Nyakaliro na Kisiwa cha Kome. Uzinduzi huo umefanyika mbele ya umati wa wananchi waliokuwa na furaha kubwa, wakiongozwa na Mbunge wao, Eric Shigongo.

Kivuko hiki kimekuja kama sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini katika maeneo ya visiwani ndani ya Buchosa. Kinatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo, hasa kwa wakazi wa Kome, Soswa, Kasalazi na maeneo jirani.

Mbunge Shigongo amesema MV Mwanza ni moja kati ya vivuko viwili alivyoviomba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuondoa kero ya usafiri inayowakabili wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu. Amemshukuru Rais Samia kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kuhakikisha huduma hiyo muhimu inawafikia.

Aidha, Shigongo ameeleza kuwa ujio wa MV Mwanza unafuatia uwepo wa vivuko vingine vilivyokwisha wasili au vinavyotarajiwa kufika, kama vile MV Sengerema, MV Kome II na III, hatua inayodhirisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha maisha ya wananchi wa maeneo ya pembezoni kwa kuwapatia huduma bora za usafiri.

Wananchi wa Buchosa wameonyesha furaha yao kwa nyimbo, ngoma na shangwe wakieleza kuwa kivuko hicho ni mkombozi mkubwa katika shughuli zao za kila siku, hasa wakulima, wavuvi na wafanyabiashara wa visiwani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii