RAIS wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kukutana na viongozi kutoka mataifa matano ya Afrika wiki ijayo kwa ajili ya majadiliano ya kibiashara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Bara la Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, White House, Trump atakutana na viongozi wa Gabon, Guinea-Bissau, Liberia, Mauritania na Senegal mnamo Julai 9, ambapo watajadili fursa za kibiashara na kushiriki chakula cha mchana katika Ikulu hiyo.
Taarifa hizo zinathibitisha ripoti za awali zilizotolewa na majarida ya Africa Intelligence na Semafor, ambazo zilieleza kuwa mkutano huo wa kilele utafanyika kuanzia Julai 9 hadi 11 mjini Washington.
Afisa mmoja wa White House amesema kuwa Rais Trump anaamini Bara la Afrika lina fursa kubwa za kiuchumi ambazo zinaweza kuwa na manufaa ya pande zote kwa Wamarekani na kwa mataifa ya Afrika.
Hata hivyo, tangu aingie madarakani, Trump amekuwa akikosolewa kwa baadhi ya sera zake zinazodaiwa kudhoofisha uhusiano kati ya Marekani na Afrika, ikiwamo hatua ya kupunguza kwa kiasi kikubwa misaada ya maendeleo kwa mataifa ya bara hilo.