Wakili azua gumzo mitandao

MAHAKAMA KUU ya Gujarat nchini India imeanza kusikiliza kesi dhidi ya wakili wake mmoja, Bhaskar Tanna, baada ya video inayomuonesha akinywa bia na kuzungumza kwenye simu wakati wa kikao cha mahakama kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Video hiyo ya sekunde 15 ilizua mjadala mkali mtandaoni, huku watumiaji wengi wa mitandao wakihoji nidhamu ya mawakili wanapokuwa katika mazingira ya kazi.Wakili Tanna alionekana akiwa kwenye kikao cha kimahakama kwa njia ya mtandao huku akinywa kile kinachoaminika kuwa bia, jambo lililowashangaza wengi.

Mahakama Kuu ya Gujarat ilieleza kuwa kitendo hicho kinaashiria dharau kwa chombo hicho cha haki, hivyo ikaamuru hatua kali zichukuliwe dhidi ya wakili huyo. 

Pamoja na agizo hilo, mahakama ilimuagiza Msajili kutoa onyo rasmi kwa Wakili Tanna na kumzuia kushiriki tena katika kesi aliyokuwa akiihudhuria kwa njia ya mtandao.

Akijitetea mbele ya jopo la majaji wawili, Wakili Tanna alieleza kuwa kitendo hicho kilitokea kwa bahati mbaya alipobonyeza kitufe cha video badala ya sauti.

Aliongeza kuwa aliiomba mahakama msamaha bila masharti mara mbili, na kusisitiza kuwa tukio hilo halikutokea wakati usikilizwaji wa kesi ukiendelea, bali baada ya kuhitimishwa kwake.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudharau Mahakama ya mwaka 1971 nchini India, mtu yeyote anayefanya kitendo kinachoonekana kuidharau mahakama anaweza kuhukumiwa kifungo kisichozidi miezi sita, kutozwa faini au adhabu zote mbili kwa pamoja.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii