Vilio na simanzi kwa ndugu waliofika KCMC kupokea miili ya waliopoteza maisha ajili ya Same

Vilio na simanzi vimetawala katika viwanja vya Hospitali ya KCMC, mkoani Kilimanjaro wakati ndugu wakishuhudia majeneza 36 kati ya 42 yenye miili ya ndugu zao waliofariki dunia ajalini baada ya magari mawili kugongana na kuwaka moto Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. 

Katika uwanja huu wa Hospitali ya KCMC zipo meza maalumu kwa ajili ya kuweka majeneza yenye miili ya watu 36 kati ya 42 ambao wataagwa kimkoa na kisha kukabidhiwa familia kwa taratibu za maziko.


Ndugu hao pamoja na waombolezaji wengine ambao walianza kuwasili saa 3 asubuhi  Julai 3, mwaka huu katika viwanja hivyo ambapo wameshindwa kujizuia huku wakibubujikwa na machozi baada ya kuona majeneza yenye miili ya ndugu zao yakishushwa kwenye magari ya polisi.

Aidha kutokana na wingi wa majeneza, miili hiyo imekuwa ikiletwa awamu kwa awamu katika viwanja hivyo kwa ajili ya taratibu za kuaga na kisha kukabidhiwa kwa ndugu.

Kila majeneza yalipokuwa wakishushwa katika magari na kwenda kuwekwa eneo maalumu lililoandaliwa, vilio kutoka kwa waombolezaji viliongezeka. 

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu alisema waliofariki kwenye Coaster ni watu 31 ambao kati yao wanawake ni 21 na wanaume ni 10, huku kwenye basi la Chanel one wakifariki watu 11 na hivyo kufanya jumla ya waliofariki kufikia 42.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la upande wa kulia wa basi la Chanel One na dereva kukosa mwelekeo kisha kushindwa kulimudu gari na kuhama upande wa kulia wa barabara na kisha kugongana uso kwa na Coaster na kusabbaisha kuwaka moto.


Ikumbukwe kuwa ajali hiyo ilitokea Juni 28, mwaka huu katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso.




Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii