Kiongozi wa China Xi Jinping amemwambia mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwamba usitishaji mapigano katika vita vya Iran na Israeli ni "kipaumbele kisichozuilika," vyombo vya habari vya serikali ya China vimeripoti siku ya Alhamisi, vikinukuu mazungumzo ya simu kati ya viongozi hao wawili.
Kiongozi wa China Xi Jinping ametoa wito kwa pande zote, hasa Israeli, kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo ili kuepusha kuongezeka mara kwa mara kwa hali hiyo na kuzuia kwa uthabiti kuenea kwa vita.
Viongozi hao wawili "wamelaani vikali" mashambulizi ya Israeli nchini Iran, wakitaka kutatuliwa kwa mzozo wa kisiasa na kidiplomasia, Kremlin imetangaza Alhamisi kufuatia mazungumzo ya simu kati ya marais wa Urusi na China.
Paris yataka "raia wote wa Ufaransa wanaotaka kuondoka Iran kfahamisha haraka iwezekanavyo"
"Raia wote wa Ufaransa wanaotaka kuondoka Iran wanaalikwa kuripoti haraka iwezekanavyo kwa ubalozi wetu," amesema Jean-Noël Barrot, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi asubuhi. "Timu zimetumwa kwenye mpaka wa Uturuki na Armenia ili kuwezesha taratibu za kibalozi."
Nchini Israeli, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ametoa wito kwa Wafaransa kutumia "tahadhari." "Wale wanaotaka kurejea Ufaransa wanaweza kufanya hivyo kwa barabara hadi Jordan na Misri, nchi ambazo kuna urahisi wa kusafiri kwa ndege."
Wakati huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema kuwa atakutana na wenzake wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, mjini Geneva siku ya Ijumaa, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran. Amesema mkutano huo utafanyika kwa ombi la Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kundi la "E3," ambalo lilikuwa miongoni mwa wapatanishi wa makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015.