Katika mnada wa hivi karibuni, bei ya juu ilikuwa Sh 2,710 na bei ya chini ilikuwa Sh 2,510 kwa kilogramu moja. Tani 3,000 ziliingizwa sokoni na kushindaniwa na wanunuzi.
Mkulima wa ufuta kijijini Ruhokwe, Kata ya Mnolela katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Lindi, Kasssim Cosmas anasema ameridhishwa na bei hiyo ya Sh 2,710 na bei ya chini ya Sh 2,510 ya mauzo ya ufuta ghafi kwa kilogramu moja.
Akizungumzo na gazeti la HabariLEO katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mnolela ulipofanyika mnada wa kwanza, anaomba serikali iangalie zao hilo kwa kutoa misaada mbalimbali ili wakulima wazalishe kwa wingi na kwa tija zaidi kama ilivyo katika mazao mengine likiwamo korosho.
Anasema kwa mtazamo wake, uzalishaji katika msimu wa 2025/2026 unaweza kupungua katani hapo kutokana na ugonjwa wa ukaukaji mmea. Diwani wa Kata ya Mnolela ambaye pia ni mkulima wa ufuta na korosho kijijini Mnolela, Omary Liveta anasema wakulima wanapaswa kuthamini mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa ndio mkombozi.
Anasema mfumo huo unawezesha na kusaidia upatikanaji wa soko la uhakika na bei nzuri yenye tija huku ukiwakutanisha wakulima na wanunuzi kwa njia ya mnada. Anasema hatua ya serikali kusimamia ushirika inathibitishia nia njema ya kuwafanya wafanikiwe kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kinachohudumu katika halmashauri za Kilwa, Mtama na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Noordin Swallah anasema tani 3,000 za ufuta ghafi ziliuzwa katika mnada wa kwanza unaosimamiwa na soko la bidhaa, Mamlaka ya Mazao Mchanganyiko (COPRA) na vyama vikuu vya ushirika vya Lindi Mwambao na Runali.
Chama hicho kinatoa huduma zake katika wilaya za Nachingwea, Liwale na Ruangwa mkoani Lindi. Anasema wakulima wamekubali bei ya juu iliyouzwa ya ufuta ghafi ya Sh 2,710 na bei ya chini ya 2,510 baada ya kutokea ushindani miongoni mwa wanunuzi kwa njia ya mnada.
Anasema lengo la chama kikuu cha ushirika ni kukusanya tani 36,000 za ufuta ghafi kupitia wakulima wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mtama na Kilwa mkoani Lindi. Katika taarifa kuhusu tathmini ya kilimo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa Lindi (Uchumi na Uzalishaji), Mwinyijuma Mkungu anasema katika msimu wa 2024/2025 Mkoa wa Lindi ulikusanya na kuuza kilogramu 68,254,850 za ufuta ghafi.
Anasema ufuta ghafi uliuzwa kwa Sh 234,827,565,024 katika msimu wa 2024/2025 kupitia minada 17 iliyosimamiwa na vyama vikuu vya ushirika vya Runali na Lindi Mwambao. Kwa mujibu wa Mkungu, lengo ilikuwa kukusanya kilogramu 61,102,500.
“Kwa msingi huo, uzalishaji wa ufuta katika kipindi hiki ulivuka lengo kwa kufikia asilimia 111,” anasema. Ofisa Uendeshaji Biashara katika Soko la Bidhaa (Tmx), Mahama Kadikilo anasema mnadani hapo mbele ya maofisa ushirika wa wilaya na mkoa kuwa, wanunuzi wameshindana na kufikia bei ya juu Sh 2,710 na chini ya Sh 2,510 kwa ajili ya ufuta ghafi katika mnada wa kwanza.
Anasema ufuta ghafi ulikusanywa kwenye maghala ya Buko katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi; Hazina na Ilulu yaliyo katika Halmashuari ya Mtama wilayani Lindi na Nangurukuru wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Kamishina wa Ushirika Kitaifa, Zainab Telack anawataka wakulima kusimamia na kulima ufuta mweupe akisema unahitajika zaidi sokoni. Anawahimiza kuacha kasumba ya kuuza mazao yao kinyemela kwani kufanya hivyo ni kujiibia wenyewe na kujitia hasara.