VIKAO VYA MABALOZI WA KIMATAIFA KUANZA KUFANYIKA DODOMA KUANZIA JUNI 2025

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa kwa kuwa ofisi za wizara yake zinatarajiwa kuhamia rasmi Makao Makuu ya Nchi Dodoma ifikapo Juni 2025 atahakikisha kuwa vikao vyote vya mabalozi kutoka mataifa mbalimbali vinafanyika jijini Dodoma badala ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa awali.

Waziri Kombo amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha hadhi ya Dodoma kama kitovu cha maamuzi ya kitaifa na kimataifa sambamba na kuonyesha utayari wa mkoa huo katika fursa za diplomasia ya uchumi.

Ametoa kauli hiyo Mei 27, 2025 jijini Dodoma katika mkutano maalumu uliolenga kuwakutanisha mabalozi kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili fursa za uwekezaji zilizopo Dodoma.

Waziri Kombo ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuifanya diplomasia ya uchumi kuwa nyenzo kuu ya kukuza ushirikiano wa kimataifa na kuvutia wawekezaji wa kimkakati.

Amesema kuwa kuhamia kwa wizara hiyo na taasisi muhimu Dodoma kutasaidia kujibu maswali kuhusu utayari wa mkoa huo kupokea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kidiplomasia na kiuchumi za kitaifa na kimataifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii