Msajili mkuu wa Vyama vya siasa nchini Tanzania ametangaza kusitisha kutoa ruzuku kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hadi pale watakapotekeleza maelekezo ya Ofisi ya Msajili kutokana na Msajili huyo kusema Chama hicho hakina Viongozi wanaoweza kusimamia mapato na matumizi ya marejesho ya fedha za Umma ambapo hatua hii inakuja siku mbili tangu Kamati Kuu ya CHADEMA iazimie kuwa haitofuata uamuzi wa Msajili kwa kutengua uteuzi wa Wajumbe wanane wa Sekretarieti na Kamati Kuu ya Chama hicho waliothibitishwa na Baraza Kuu la Chama hicho January 22,2025.
Taarifa hiyo ilitolewa May 27,2025 na Ofisi ya Msajili wa Vyama huku akisema kutokana na ombi la uongozi lililopo CHADEMA Msajili kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 18(6) cha Sheria ya Vyama vya siasa ameamua kusitisha kuwapa ruzuku CHADEMA hadi watakapotekeleza maelekezo ya Msajili wa Vyama vya siasa kwa sababu Chama hicho hakina Viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha za umma.
Aidha majibu ya CHADEMA yalikuja kufuatia baada ya Msajili kukiandikia Chama hicho kutokana na aliyekuwa Mwenyekiti CHADEMA Wilaya ya Mwanga Lembrus Mchome kumuomba Msajili kutengua maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho kwakuwa kikao kilikuwa na kasoro.
Nakuendelea kusema kuwa Baraza kuu halikuwa halali kwani akidi haikutimia lakini pia ndani yake kulikuwemo na Watu ambao sio Wajumbe halali wa Baraza kuu kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, kauli ambayo CHADEMA imeipinga na hivi karibuni Meya wa zamani wa Ubungo Boniface Jacob alinukuliwa akisema Mchome amepangiwa nyumba ya kuishi Masaki na Msajili hivyo mpango wao ni mmoja unaolenga kuivuruga CHADEMA.