Serikali yaweka mpango wa kutangaza ajira mpya 45,000 hivi karibuni

Serikali imesema kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha itakuwa imetangaza nafasi za ajira mpya 45,000 kwa kada mbalimbali ambazo utekelezaji wake unafanyika.

Mwaka wa fedha wa Serikali unakwisha Juni 30 ya kila mwaka hivyo kwa kauli hiyo kuna nafasi za ajira zitakazotolewa ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne Mei 27, 2025 na Naibu Waziri, Deus Sangu ambaye amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 Serikali imeidhinisha jumla ya nafasi 41,500 za ajira mpya kwa kada mbalimbali ambazo zitawalenga kuajiri wahitimu stahiki.

Naibu waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga ambaye ametaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa ajira kwa wahitimu wa vyuo nchini.

Sangu amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetoa nafasi 47,404 za ajira mpya kwa kada mbalimbali ambazo utekelezaji wake unaendelea kupitia sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma na mamlaka nyingine na wasailiwa kutoka vyuo mbalimbali waliofaulu wamepangiwa vituo vya kazi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii