WANANCHI WATAKIWA KUWA WAZALENDO WA NCHI YAO

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa  ametoa wito kwa wananchi kuonyesha uzalendo kwa kutokubali kwa namna yoyote ile kutumika au kushiriki katika njama yoyote ya kuisaliti nchi yao kwa kutoruhusu wageni wanaoingia nchini kwa vibali halali lakini baadaye kujichanganya na jamii kisha kuanza kufanya shughuli zisizoruhusiwa jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za nchi.

Akizungumza leo Jumatatu, Mei 26, 2025 bungeni jijini Dodoma Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2025/26,

Bashungwa amesema kushikamana na kulinda nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje ni jambo la muhimu kwa Watanzania huku akisisitiza kuwa adui wa Taifa katika karne ya 21 si lazima atumie vifaru bali anaweza kutumia njia nyingine zenye madhara makubwa kwa jamii.

Aidha amefafanua kuwa Serikali haitakubali kuona amani na utulivu wa nchi vikihujumiwa, na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi salama kwa raia wake.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii