Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Hashim Rungwe amesema hana tatizo lolote kupokea msaada kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) endapo utatolewa kwa nia njema akisisitiza kuwa siasa si uadui bali ni jukwaa la kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Rungwe amesema yapo maneno mengi mtaani yanayomuhusisha na CCM lakini ukweli ni kuwa hadi sasa hajapokea msaada wowote kutoka chama hicho tawala hata hivyo amesisitiza kuwa endapo CCM itaamua kumpa msaada hataona tatizo kuukubali.
Rungwe amesema kuwa amesikia tetesi zinazozagaa kuhusu Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Freeman Mbowe kutaka kujiunga na chama chake huku akisisitiza kuwa milango ya Chaumma iko wazi kwa yeyote mwenye nia ya kujiunga.
Aidha ameeleza kwamba hajamsikia Mbowe mwenyewe akieleza wazi nia hiyo ya kujiunga na Chama hicho lakini iwapo ataamua kujiunga chama kipo tayari kumpokea akiwa kama mwanacha mpya.