Kamati Kuu ya CHADEMA, imeazimia kuwa haitofuata maamuzi ya Msajili mkuu wa Vyama vya siasa ambayo pamoja na mambo mengine yaliyolenga kutengua uteuzi wa Wajumbe wanane wa Sekretarieti na Kamati Kuu ya CHADEMA waliothibitishwa na Baraza Kuu la Chama hicho January 22, 2025, kwakuwa maamuzi hayo ya Msajili ni batili.
Akiongea Jijini Dar es salaam May 25,2025, Makamu Mwenyekiti Bara John Heche amesema Kamati Kuu yetu ya Chama imekutana kwa siku mbili May 23 na May 24,2025 na haya ni maazimio ya Kamati Kuu moja imepokea barua ya Msajili wa Vyama iliyoandikwa kwa Katibu Mkuu wa Chama chetu na kutafakari kwa kina na imejiridhisha kwamba Msajili amekwenda kinyume na Sheria ya Vyama vya siasa kwasababu hana mamlaka ya kupokea, kusikiliza na kufanyia maamuzi malalamiko ya Mwanachama wa Chama chochote cha siasa kama alivyofanya hivi sasa, maamuzi yake ni batili na CHADEMA haitofuata hayo maamuzi yake.
Majibu ya CHADEMA yamekuja kufuatia mara baada ya Msajili kukiandikia Chama hicho kwa Mwenyekiti CHADEMA Wilaya ya Mwanga Lembrus Mchome kumuomba Msajili kutengua maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho kwakuwa kikao kilikuwa na kasoro akisema Baraza kuu halikuwa halali lakini pia ndani yake kulikuwemo na Watu ambao sio Wajumbe halali wa Baraza kuu kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, kauli ambayo CHADEMA imeipinga na hivi karibuni Meya wa zamani wa Ubungo Boniface Jacob alinukuliwa akisema Mchome amepangiwa nyumba ya kuishi Masaki na Msajili hivyo mpango wao ni mmoja unaolenga kuivuruga CHADEMA.