Kiongozi wa Mapinduzi Gabon Jenerali Nguema Ashinda Uchaguzi

Brice Oligui Nguema, ambaye mwaka 2023 aliongoza mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Ali Bongo, ameshinda rasmi uchaguzi wa rais wa Jumamosi kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura, kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa.

Nguema, ambaye alipindua utawala wa familia ya Bongo iliyotawala kwa karibu miaka 60, sasa ameimarisha nafasi yake ya kuendelea kuongoza taifa hilo la Afrika ya Kati.

Hata hivyo, uchaguzi huo umetajwa na wakosoaji kuwa na mazingira yaliyoandaliwa kwa maslahi ya Nguema mwenyewe, kwa kile walichosema katiba mpya na kanuni za uchaguzi kubuniwa kumpa njia rahisi ya kushinda. Vigogo wengi wa upinzani waliotajwa kuwa na uwezo wa kumpa upinzani mkubwa walitengwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Katika uchaguzi huo, Jenerali Nguema mwenye umri wa miaka 50, alikabiliana na wagombea wengine saba, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Alain Claude Bilie-by-Nze, aliyewahi kuhudumu chini ya utawala wa Ali Bongo, pamoja na vinara wa chama tawala cha zamani cha PDG, Stéphane Germain Iloko na Alain Simplice Boungouères.

Ushindi huo unaifanya serikali yake kuendelea na awamu mpya ya uongozi katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta, huku ikikabiliwa na presha ya kidemokrasia kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na wananchi wanaotamani mabadiliko.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii