Vijana takribani 132 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 22 kutoka mikoa mbalimbali, hasa ya pembezoni mwa Tanzania, wamekutwa huko Mlandizi, Kibaha Vijijini, mkoani Pwani, wakijihusisha na biashara ya mtandaoni ambayo inadaiwa kuwa ya kitapeli kutokana na kufanyika kwenye mazingira ya usiri chini ya kampuni ya QI Group of Company inayodaiwa kuwa na makao makuu yake nchini Malaysia.
Februari 14, majira ya saa tatu usiku mpaka saa saba usiku, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Salim Morcase, akiwa na maafisa wengine pamoja na askari, walifanya ufuatiliaji na msako wa kushtukiza na kufanikiwa kuwakuta vijana hao pamoja na viongozi wao kwenye nyumba tatu tofauti, ambako hukusanyika kwa shughuli zao hizo.
Kamanda Morcase amebainisha kuwa mafanikio ya kukamatwa kwa vijana hao yametokana na taarifa za kiintelijensia, ambapo walikuwa wakijihusisha na shughuli ambazo hazina mwelekeo mzuri na pia zina viashiria vya upatu, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Ameongeza kuwa baadhi ya viongozi wa mtandao huo wamekamatwa na watafanyiwa mahojiano, na uchunguzi zaidi utafanyika, kisha taratibu za kisheria zitachukuliwa.