Hamas yapinga mapendekezo ya Trump kudhibiti Gaza na kuwaondoa raia

Wapiganaji wa Hamas wamelaani vikali matamshi ya rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mipango yake ya kuidhibiti Gaza na kuwahamishia wakaazi katika mataifa mengine iwapo wanataka kuondoka au la.

Trump alitoa kauli hii kuhusu Gaza wakati wa kikao na wanahabari pamoja na mgeni wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katika Ikulu ya White House.

Kauli ya Trump pia imepokea hisia mseto baadhi wakiunga mkono mapendekezo yake wakati wengien wakiyapinga.

Afisa wa Hamas kwa upande wake ametaja matamshi ya Trump kama ya kushangaza na ya kijinga.

Aidha Hama inasema mpango wa Trump ambao umetajwa kuwa wakibaguzi unalenga kuwaondoa raia wa Palestine katika makazi yao.

China kwa upande wake kupitia Wizara yake ya mambo ya kigeni imepinga mpango unaolenga kuwaondoa wakazi wa Gaza katika eneo lao kwa nguvu.

Spika wa bunge la Marekani Mike Johnson, mwanachama wa Republican amesifia mpango wa Trump kuhusu Gaza anaosema unalenga kuleta amani ya kudumu katika Ukanda huo.

Naye Chris Murphy, Seneta aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Democratic ametaja matamshi ya Trump kama mzaha.

Mwenzake Chris Van Hollen naye pia amesema mpango huo wa Rais Trump kuwaondoa raia wa Gaza ni kitendo cha kuwalenga watu kwa misingi ya kikabila.

Hatua hiyo ya Trump pia imekashifiwa na kupingwa na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese.

Saudi Arabia, mshirika wa karibu wa Palestine na mpatanishi katika mzozo wa Hamas na Israel imesema hakuna uhusiano na Israeli bila ya kuwepo kwa taifa la Palestine.

Katika hatua nyengine, Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio amepongeza mpango wa bosi wake rais Trump.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii