NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki amemwambia mtangulizi wake Rigathi Gachagua kuwa kauli yake kwamba Rais William Ruto atakuwa rais wa muhula moja ni ndoto na halitakuwa jambo rahisi kutimiza.
Ubabe kati ya Profesa Kindiki na Bw Gachagua unaendelea kutikisa Mlima Kenya huku siasa za uchaguzi wa 2027 zikiendelea kushika kasi.
Mnamo Jumatatu wakati wa ufunguzi wa afisi mpya za DAP-Kenya, Bw Gachagua alitangaza wazi kuwa lengo lake ni kuweka muungano dhabiti wa kisiasa ambao utampeleka Rais Ruto nyumbani mnamo 2027.
Hata hivyo, Jumatano alijibiwa na Profesa Kindiki aliyemwambia hilo ni jambo gumu kabisa kwa sababu Rais naye anamakinikia kuchapa kazi ili Wakenya wamchague tena mnamo 2027.
“Usitutishe kuwa utahakikisha tunahudumu kwa muhula moja pekee. Nimewaona baadhi ya watu wakisema lengo lao ni kuhakikisha William Ruto ni rais wa muhula moja. Hiyo inaweza kuwa motisha kwao kivipi kama kiongozi?
“Rais Ruto kwa kudura za Mwenyezi Mungu amebahatika kuwa kati ya Wakenya watano ambao wamehudumu kama rais wa nchi,” akasema Profesa Kindiki.
Alikuwa akiongea jana katika makazi ya naibu rais mtaani Karen alipokutana na viongozi kutoka kaunti yake ya Tharaka-Nithi.
Ujumbe huo ulijumuisha Gavana Muthomi Njuki, wabunge Patrick Munene (Chuka/Igamba’ngombe), Gitonga Murugara (Tharaka) na Kareke Mbiuki (Maara) pamoja na Seneta Gataya Mwenda na Mbunge Mwakilishi wa Kike Susan Ngugi.
Profesa Kindiki alisema lengo la Bw Gachagua na baadhi ya wanasiasa wa upinzani litakuwa ngumu kutimiza na badala yake wanastahili kujiuza kwa kusema kile ambacho watawafanyia Wakenya wakifanikiwa 2027.
Naibu Rais aligusia baadhi ya miradi mikuu ya Rais Ruto akirejea Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHA) ambayo alikiri kuwa huenda si maarufu kwa Wakenya kutokana na changamoto ambazo zimeshuhudiwa kwenye hatua ya mwanzo ya utekelezaji wake.
Aliulinganisha utawala wa miaka miwili wa Rais Ruto na ule wa Mwai Kibaki (marehemu) ambao ulikumbana na changamoto tele hadi akashindwa kwenye kura ya maamuzi ya kubadilisha katiba 2005 na akalazimishwa kuvunja baraza lake la mawaziri.
“Licha ya changamoto hizo, Kibaki aliwajibikia Wakenya na kazi yake inasifiwa hadi leo. Rais Ruto anaandamwa na changamoto kama hizo lakini amesalia imara katika nia yake ya kubadilisha Kenya,” akaongeza Profesa Kindiki.
“Hata kama Rais hatachaguliwa kwa mara ya pili lakini akabadilisha maisha ya Wakenya kwenye sekta ya afya, uchumi, elimu, nyumba na kubuni nafasi ya ajira kwa vijana, atakuwa ametimiza malengo yake. Kwa hivyo, usitutishe na urais wa muhula moja,” akasema.
Kiongozi huyo pia alisema ameamua kuanza kumkabili Bw Gachagua ana kwa ana katika eneo la Mlima Kenya na wikendi hii atakuwa Kaunti ya Embu ambapo alisema ataongoza mkutano mkubwa wa zaidi ya watu 20,000.
Hivi majuzi Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alimshutumu Profesa Kindiki kwa kutelekeza eneo la Mlima Kenya na kulikwepa kwa kuhofia ghadhabu za raia.
Jana, Profesa Kindiki alisema kuwa hatakuwa akimpinga rais jinsi ambavyo baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya wanavyomsukuma akisema kuwa anafahamu kazi yake ya kuhakikisha Wakenya wanahudumiwa.
Pia alimtaka Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ajiuzulu na kuungana na upinzani badala ya kupinga serikali ile ile ambayo anaihudumia.