Shirika la ndege la Ubelgiji lasitisha safari zake kwenda na kutoka DRC

Shirika la ndege la Ubelgiji limetangaza kusitisha safari zake za leo Jumatano kwenda na kutoka jijini Kinshasa kutokana na machafuko yalioshuhudiwa kwenye eneo hilo.

Uharibifu wa mali uliripotiwa Kinshasa wakati wa maandamano yalioongozwa na raia wenye hasira kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama mashariki ya DRC.

Shirika hilo linasema litatangaza wakati wa kurejelewa tena kwa safari hizo baada ya kuangazia kwa umakini hali ya usalama.

Shirika hilo huwa na safari za kila siku Kutoka Brussels hadi Kinshasa na kurejea kwenda Brussels.

Maandamano huko Kinshasa yalitokana na kile waandamanaji walisema ni hatua ya jamii ya kimataifa kuendelea kusalia kimya kutokana na utovu wa usalama mashariki ya DRC na yalisababisha uvamizi katika balozi wa Rwanda, Kenya, Uganda, UfaransaMarekani na Ubelgiji.

Maduka ya jumla pia yaliporwa wakati wa maandamano hayo, magurudumu ya magari yakichomwa moto, usafiri pia ukitatizika.

Mataifa ya Ufaransa, Kenya pamoja na Umoja wa Ulaya yalilaani uvamizi kwenye balozi zake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii