Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Ghebreyesus, ameipongeza Tanzania kwa kuchukua hatua za haraka katika masuala ya afya mkoani Kagera hasa ya ugonjwa unaoshukiwa kuwa Marburg, akibainisha kuwa WHO ilipokea taarifa za hatua hizo, jambo ambalo ni muhimu kwa afya ya jamii.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya mtandao kupitia Zoom, YouTube, na LinkedIn siku ya tarehe 16 Januari 2025, Dkt. Tedros ametoa muhtasari wa masuala ya afya duniani na kugusia hali ya afya katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania
Amesema serikali imepeleka timu ya taifa ya dharura (National Response Team), maabara zinazotembea, pamoja na vitengo vya matibabu kwa ajili ya kushughulikia hali hiyo, na kusisitiza utayari wake wa kutoa msaada wowote unaohitajika ili kuhakikisha changamoto hiyo inakabiliwa kikamilifu.
Aidha, Dkt. Tedros ameishauri Serikali ya Tanzania kuhakikisha sampuli zilizokusanywa mkoani Kagera zinapelekwa kwenye maabara za rejea za kimataifa kwa uchunguzi wa kina, pamoja na kukusanya sampuli za ziada kwa kuzingatia taratibu za kawaida za afya ya umma.
Pia, ameipendekeza Serikali kuimarisha ufuatiliaji wa washukiwa wa ugonjwa husika kwenye mipaka ya mkoa huo, sambamba na kushirikiana na nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kubaini na kutibu washukiwa wa ugonjwa huo.