Mamlaka nchini Korea Kusini zimejikuta katika mgogoro mkubwa na kikosi cha usalama cha Rais aliyeondolewa Madarakani Yoon Suk-yeol baada ya maafisa usalama na uchunguzi kufika kwenye nyumba ya rais aliyeondolewa madarakani ili kutekeleza hati ya kukamatwa kwake kutokana na tuhuma zinazomkabili.
Maafisa wa kupambana na rushwa nchini humo walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Kikosi cha Ulinzi wa Rais (PSS) baada ya kujaribu kuingia katika makazi ya Yoon huko Seoul mapema leo Ijumaa asubuhi ili kumkamata kiongozi huyo aliye katika hali ngumu.
Mkuu wa Kikosi cha PSS, Park Jong-joon, alizuia kuingia kwa maafisa kutoka Ofisi ya Uchunguzi wa Rushwa kwa Maafisa wa Juu (CIO) baada ya kupita vizuizi katika maeneo yaliyo salama, kama ilivyoripotiwa na Shirika la Habari la Yonhap.
“Waendesha mashtaka na wachunguzi wa CIO wamezuiwa kumkamata rais na Kikosi cha Usalama wa Rais mbele ya makazi ya rais baada ya kupita vizuizi vya kwanza na vya pili,” Yonhap ilimnukuu afisa wa polisi akisema.