Idara ya Uhamiaji nchini imetakiwa kuimarisha udhibiti wa Wahamiaji haramu na baadhi ya wageni wanaoingia na kufanya biashara haramu huku wakiwa na lengo lililojificha la kuvunja amani yetu kukamatwa na kuwachukulia hatua kali za kisheria pindi wanapobainika
Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Dkt. Tulia Akson katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi la Jengo la Afisi za Uhamiaji Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja Desemba 29, 2024
Dkt.Tulia amesema usafirishaji haramu wa binadamu umekuwa ukipigwa vita duniani na hapa nchini hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kupambana nalo ili kuweza kulitokomeza kabisa.
“Kwa kusema hayo ndugu zangu hatua tumepiga ni kweli lakini tunataka hatua ipigwe zaidi hasa katika hili eneo la Uhamiaji kwanini kwasababu wako wale watu huwa wanaitwa wahamiaji haramu tunatamani waendelee kudhibitiwa, kwakweli mnafanya kazi kubwa sana lakini muendelee kuifanya vizuri zaidi ili nchi yetu iendelee kuwa salama”.Alisema Dkt. Tulia
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo akimuwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Idara ya Uhamiaji imeboresha njia za kielektroniki katika huduma zote za kiuhamiaji.
“Idara ya Uhamiaji Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo ambapo imefanikiwa kuweka mifumo ya kielektronikia katika utoaji wa huduma zote za kiuhamiaji kwa nchi nzima kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar”. Amesema Sillo
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania CGI Dkt. Anna Makakala amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha na kuiamini Idara ya Uhamiaji kwa kuboresha miundo mbinu na maslahi ya Watumishi, Maafisa na Askari wa Uhamiaji.
Mradi huo wa ujenzi wa jengo la Afisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 1.8 ambapo umefikia asilimia 85% za utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Aprili 2025 ukiwa unatarajiwa kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za Uhamiaji kwa raia, wawekezaji na Wageni.