Rais wa Sierra Leone asaini sheria inayopiga marufuku ndoa za utotoni

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio Jumanne alitia saini sheria inayopiga marufuku ndoa za utotoni katika nchi ambako maelfu ya wasichana wanaolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

“Wanawake wetu wamepata uhuru, Bio alisema wakati wa hafla iliyoandaliwa na makundi ya wanawake na wake wa marais wa Afrika Magharibi katika mji mkuu Freetown.

Bunge la Sierra Leone mwezi uliopita liliidhinisha sheria hiyo, kwa kupasisha mswaada ambao unafanya kuwa kosa la jinai kuwaoa wasichana wenye umri ulio chini ya miaka 18 na kufungwa jela angalau miaka 15 na kulipa faini ya zaidi ya dola 2,000.

“Haya ni mafanikio ambayo yataonyesha utendaji kazi wa utawala wetu,” alisema Bio, akiitaja sheria hiyo kuwa “mwanga wa matumaini barani Afrika ambapo wanawake wanakutana na pingamizi nyingi kujiamulia mustakabali wao wenyewe na kutoa mfano mzuri kwa ulimwengu.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii