WANASAYANSI wamegundua mbinu mpya ya kutambua kansa ya matiti huku ikipunguza uwezekano wa matokeo ya kupotosha.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la chama cha rediolojia cha Amerika Kaskazini (RSNA) la Radiology: Imaging Cancer, teknolojia hiyo kwa jina Low-dose positron emission mammography (PEM), inatoa matokea bora ya utambuzi ikilinganishwa na ile ya kawaida ya mammografia.
Kwa kawaida mbinu ya mammografia hutumika katika utambuzi wa mapema wa kansa ya matiti, lakini uwezo wake wa ugunduzi unapungua katika matiti yenye uzito. Na kutokana na kuwa nusu ya watu wanaopimwa huwa na matiti yenye uzito, wengi wa wagonjwa hawa huhitaji kupimwa zaidi kupitia mbinu ya MRI, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa mammografia.
Katika utafiti huu, wanawake 25 wenye umri wastani wa miaka 52 na ambao hivi majuzi waligundulika kuugua kansa ya matiti, walifanyiwa uchunguzi wa PEM ambapo wataalam wawili wa rediolojia walikagua picha baada ya saa nne na kulinganisha matokeo ya maabara.
Yakilinganishwa na matokeo ya MRI, yale ya PEM yalitambua aina 24 kati ya 25 ya kansa, huku viwango vya matokeo ya kupotosha vikiwa asilimia 16 pekee, ikilinganishwa na asilimia 62 katika MRI.
Kulingana na watafiti, teknolojia ya PEM ina uwezo wa kushusha gharama za huduma ya afya kwani utafiti huu unaonyesha kwamba huenda ikapunguza taratibu zaidi za kimatibabu ikilinganishwaa na MRI.
Aidha, teknolojia hii imesanifiwa kutoa dozi ya tibaredio inayofanana na ile inayotolewa kwenye uchunguzi wa mamografia pasipo haja ya kubana matiti, shughuli ambayo hukosesha starehe wagonjwa.
“Katika uchunguzi huu, uwezo wa teknolojia hii kuleta matokeo bora pasipo kuzingatia uzito wa matiti, unaangazia udhaifu wa utaratibu wa mamografia, hasa katika utambuzi wa kansa katika matiti yenye uzito ambapo huenda vidonda vimejificha,” alisema Vivianne Freitas, mwandishi mkuu wa utafiti huu na profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Toronto.
Huenda teknolojia hii ikachangia pakubwa katika kufasiri matokeo ya uchunguzi wa mamogramu yasiyo na uhakika, kukagua mwitiko wa tibakemia na kutambua kiwango cha maradhi, miongoni mwa wagonjwa wapya wa kansa ya matiti.
Japo uhusishwaji wa mbinu hii katika taratibu za kimatibabu haujathibitishwa kikamilifu, Dkt Freitas asema kwamba matokeo ya mwanzo ya utafiti huu ni ya kutia moyo hasa katika kuonyesha uwezo wa kutambua kansa ya matiti inayosambaa kwenye tishu zingine, kwa kutumia dozi chache za dawa ya fluorine-18-labeled FDG, ambayo hutumika katika utambuzi wa kansa.