Polisi kuwasaka Mgambo waliomjeruhi Mama kwa kipigo

Mwanamke mmoja, Aziza Juma mkazi wa Manispaa ya Morogoro amepigwa na kujeruhiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni Askari wa Jeshi la Akiba wa Manispaa hiyo, wakimtuhumu kufanya Biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Mama huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akiendelea na matibabu amesema Askari hao walimkuta akiwa na mwenzie wameketi Dukani na walimkamata wakampakiza kwenye gari na baadae kuanza kumpiga kwa kutumia magongo, kumwagiwa maji, kumbebesha mizigo kisha kufanyisha mazoezi asiyoyaweza.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro, Dkt. Abdulaziz Abood sambamba na Viongozi wengine wa Serikali kwa nyakati tofauti walifika Wodini na kumjulia hali mama huyo na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya wahusika wa tukio hilo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, Ally Machela amethibitisha kutokea Kwa tukio hilo na amesema Jeshi la Polisi linaendelea na utaratibu wake wa kisheria na endapo itagundulika ni kweli Askari hao wa Akiba wamefanya tukio hilo, watachukuliwa hatua zaidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii