Wabunge wa Ruto kukutana na Upinzani

Serikali ya rais wa Kenya William Ruto, Jumanne, imewatangaza wabunge saba wa Kenya Kwanza watakao shiriki katika mazungumzo na upinzani unaoongozwa Raila Odinga ili kumaliza uhasama wa kisiasa kati ya pande hizo mbili.

Hata hivyo chama hicho tawala kimesema hakitashiriki mazungumzo yoyote yatakayohusu kurejeshwa kazini kwa makamishna wanne wa IEBC waliofutwa kazi na Rais Ruto pamoja na kushiriki katika harakati za ufunguaji wa seva za uchaguzi.

Majadiliano hayo si ishara ya udhaifu wala njia ya kuishinikiza serikali kukubaliana na matakwa ya wapinzani wake.

Mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika katika mfumo wa bunge, yatahudhuriwa na wabunge wa chama tawala ambao ni pamoja na Boni Khalwale, Hillary Sigei, Adan Keynan, Lydia Haika, George Murugara, Essy Okenyuri na Mwengi Mutuse.

Mazungumzo hayo yatahusu hali ngumu ya maisha, ufufuaji wa uchumi na kuundwa kwa tume ya uchaguzi IEBC na kuwepo kwa makubaliano ya kisiasa.

Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika bunge la taifa, Kimani Ichung’wa ameleeza.

“Muungano huo pia umepuuza madai ya Odinga kuwa alishinda kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022, na kukariri kuwa Odinga anahitajika kuwasilisha maombi mbele ya mahakama ya juu kufanyiwa tathmini mpya ya maamuzi yaliyotolewa dhidi ya kesi aliyoiwasilisha kupinga ushindi wa rais Ruto, na kwamba msisitizo wa kufungua seva za tume ya uchaguzi ni suala lisilofikirika kwa sasa.”

Ichung’wa alisema upinzani umewasilisha mapendekezo saba katika mazungumzo kati yake na serikali ya Ruto ikiwa pamoja na hatua za haraka za kupunguza bei za unga, umeme na mafuta na ada za shule, na kutaka ukaguzi wa kitaalamu wa seva zinazotumiwa na IEBC kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa urais 2022, mapitio ya uteuzi.

Na kuongeza kuwa upinzani pia umependekeza kufukuzwa kazi kwa Makamishna wa tume ya uchaguzi, ili kuimarisha na kuboresha mfumo uchaguzi ulio huru na wa haki.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii