Raila Odinga " uchaguzi hautafanyika iwapo IEBC haitimizi matwaka yake "

Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga, ametishia kutoshiriki uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, endapo tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC haitatumia daftari la wapiga kura iliyoandikwa kwa karatasi na sio kutegemea orodha ya wapiga kura iliyotayarishwa kidigitali.

Odinga, ambaye katika uchaguzi uliopita 2017 alitaka upigaji kura kufanyika kwa njia ya digitali, amesema kwamba endapo IEBC haitatumia daftari la wapiga kura la karatasi, “uchaguzi hautafanyika nchini Kenya.”

“Daftari la wapiga kura lazima litumike katika kila kituo cha kupigia kura. Hili halina mjadala na tumeambia IEBC kwamba ni lazima tuwe na daftari la wapiga kura lililotayarishwa kwa karatasi, Pamoja na majina hayo kupatikana kielektroniki ambapo wapiga kura watatambuliwa kwa alama za vidole au picha. La sivyo, hakuna uchaguzi,” amesema Odinga.

Kenya itaandaa uchaguzi mkuu mwezi ujao Agosti tarehe 9. Odinga, ambaye alitoa madai kama hayo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2017, amedai kwamba kuna njama ya kutumia karatasi za kura ambazo tayari zimejazwa kwa faida ya mpinzani wake kwa kila baadhi ya vituo vya kupigia kura.

“wamechagua vituo vya kupiga kura kama 10,000 ambazo wataweza kuingiza hizo kura mia mbili mia mbili, ili iingie pale ndipo wapate kura milioni mbili ya ziada ya uongo.” Amedai Odinga ambaye anagombea urais kwa muungano wa vyama vingi wa Azimio.

Odinga anaungwa mkono na rais wa sasa Uhuru Kenyatta na baraza lake la mawaziri

Odinga anaungwa mkono na serikali ya sasa ya raia anayeoondoka Uhuru Kenyatta, ambaye alimshutumu mnamo uchaguzi uliopita kwa wizi wa kura, na kupelekea joto kubwa la kisiasa hadi walipokutana na kufanya makubaliano ya kushirikiana kufanya kazi, maarufu nchini Kenya kama ‘handshake’.

Mpinzani mkuu wa Raila Odinga ni naibu wa rais William Ruto, ambaye amesema kwamba yupo tayari kwa uchaguzi na hana malalamishi yoyote na tume huru ya uchaguzi IEBC.

Ruto amesisitiza kwamba tume ya uchaguzi iruhusiwe ifanye kazi yake na mfumo wowote ule utakaotumika kufanikisha uchaguzi, uwe wa karatasi au elektroniki, hana shida nao.

“Hata washindani wangu wakimteua ndugu yao kuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC, sina shida bora ateuliwe kulingana na sheria na uchaguzi uwe wa huru na haki” alisema Ruto katika kikao kati ya maafisa wa tume ya uchaguzi na wagombea wote wa urais.

Tume ya uchaguzi yajibu madai ya wizi wa kura

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, imemjibu Raila Odinga, ikisema kwamba haifanyi kazi kwa kuzingatia maslahi ya mtu binafsi na haiwezi kubadilisha sheria za uchaguzi ili kutosheleza mahitaji ya mtu mmoja.

“IEBC ni tume huru, hatupokei maagizo kutoka kwa mtu binafsi, mamlaka yoyote au taasisi yoyote. Kazi yetu inazingatia katiba na sheria za Kenya,” amesema mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, akiongezea kwamba “unaweza kutofurahishwa na namna tunavyofanya kazi lakini iwapo tunafuata sheria katika kazi yetu, hatuwezi kuwa na wasiwasi. Tunafanya kazi yetu bila uoga wala mapendeleo, na kwa kuzingatia sheria.”

Chebukati amesema kwamba kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na daftari la kupiga kura, na idadi ya karatasi za kupigia kura itakuwa sawa na idadi ya wapiga kura waliosajiliwa katika kila kituo.

Mkurugenzi wa IEBC Majan H. Marjan, amesema kwamba "Tume ya uchaguzi IEBC inafanya kazi yake kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama ya juu kabisa wa mwaka 2017 kwamba daftari ya wapiga kura ambalo linastahili kuzingatiwa kabisa ni la kidigitali na daftari la karatasi litumike tu iwapo kuna hitilafu katika mfumo wa digitali." ameongezea kwamba "daftari la karatasi linachapishwa kutoka kwa lile la digitali."

Madai ya uchapishaji wa karatasi za kupiga kura kuingiliwa na wapinzani wa Odinga

Raila Odinga vile vile amedai kwamba kampuni uliyopewa kandarasi ya kuchapisha karatasi za kupiga kura ina uhusiano na wapinzani wake.

Seneta wa Bungoma Moses Wetangula ametajwa kuwahi kukutana na baadhi ya watu wenye uhusiano na kampuni ya Ugiriki ya Lykos (Hellas) SA Holdings, ambayo ilishinda zabuni ya kiasi cha shilingi bilioni 3 ya kuchapisha karatasi za kupigia kura. Zabuni ilitolewa mwezi Oktoba mwaka 2021.

Ripoti ya gazeti ya Daily Nation la Kenya, hata hivyo haiunganishi moja kwa moja, uhusiano kati ya watu ambao Wetangula alikutana nao, na kampuni hiyo. Hata hivyo, ripoti hiyo imezua mjadala mkubwa wa kisiasa nchini Kenya.

Wetangula, ambaye ni wakili, na alikuwa Rafiki mkubwa wa kisiasa wa Raila Odinga hadi walipokosana miaka michache iliyopita, ni mmoja wa maafisa wakuu katika kampeni ya naibu war ais William Ruto, na ambaye ni mshindani mkubwa wa Odinga.

Wetangula amejibu Rail ana chama chake kwamba “tunataka kuwaambia washindani wetu wanaoitwa Azimio kuacha kuonyesha wasiwasi kila mara na kila sehemu kwa sababu inaonekana kwamba Azimio wamo katika hali ya kuchanganyikiwa Pamoja na kuwa na misukosuko ndani ya chama chao na sasa wameanza kudai kwamba kuna njama za kuwaibia kura.”

Wetangula amedai kwamba Odinga ana tabia ya kulalamika katika kila uchaguzi, akitaja miaka ya 1997, 2007, 2013 na 2017.

“Nimesoma Habari zilizochapishwa vizuri na kwa makini. Sina msaidizi anayeitwa Joshua. Sina mtu yeyeote anayefanya biashara ya uchapishaji. Watu ambao wanatajwa hata siwajui,” amesema Wetangula katika taarifa kwa vyombo vya Habari.

Mwenyekiti wa IEBC atajwa katika madai hayo

Mwenyekiti ya tume ya uchaguzi Wafula Chebukati, vile vile ametajwa na wanasiasa kwamba alifanya mikutano na Wetangula na wanasiasa wengine wanaomuunga mkono William Ruto kabla ya zabuni ya kuchapisha karatasi za kupiga kura kutolewa.

“Inasikitisha sana kwamba kuna watu wanasema mambo kama hayo. Sijawahi kuketi chini na mtu yeyote kujadiliana maswala ya kutoa zabuni ya kuchapisha karatasi za kupiga kura.” Amesema Chebukati huku wanasiasa wanomuunga mkono Raila Odinga wakitaka taasisi za serikali kufanya uchunguzi wa haraka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii