Katika
kitabu chake mashuhuri cha Sapiens, mwanahistoria Yuval Noah Harari,
anaeleza kuhusu kwanini binadamu amepiga hatua kubwa kimaendeleo
kulinganisha na wanyama wengine. Sababu anazotoa ni mbili tu; uwezo wa
kushirikiana kufanya kazi kwa idadi kubwa na kwa maelewano na pili uwezo
wa kuumba kitu ambacho huenda hakishikiki wala kuonekana lakini
kinaaminika.
Nchi
ya Tanzania ni mojawapo ya 'uumbaji' uliofanywa na mwanadamu. Miaka 100
iliyopita, eneo ambalo leo nchi hiyo ipo lilikuwepo lakini jina hilo
halikuwepo. Wakati Watanzania wakijiandaa kutimiza miaka 60 ya Uhuru wa
Tanganyika Desemba 9 mwaka huu -ni wakati mzuri sasa kutazama ni mambo
ambayo yameifanya Tanzania kuwa hivi ilivyo leo.
Kabla ya Tanzania, kabla ya Tanganyika
Kwa
wanasayansi, Tanzania ni mojawapo ya maeneo ambako inatajwa wanadamu
walianza kuishi kuliko mahali pengine duniani. Katika utafiti uliofanywa
na Mary Leakey katika eneo la Laetoli, mkoani Arusha, kuna ushahidi
kuwa watu wa zama za kale waliojulikana kwa jina la Australopithecus
afarensis waliishi hapo zaidi ya miaka milioni 3 iliyopita.
Msafiri wa Kiarabu, Ibn Battuta, aliandika katika maandishi yake ya karne ya 14 kuhusu mji wa Kilwa ulioko Lindi ambako aliueleza kama mojawapo ya miji mizuri zaidi aliyowahi kuiona katika safari zake duniani kote.
Hata mwanafalsafa wa Kiyunani, Ptolemy, katika kitabu chake cha Jiografia, ameeleza kwa kina kuhusu mji aliouita Raphta ulioko katika eneo la Azania akieleza ulikuwa na sifa zote za kuwa mji. Haijajulikana kwa yakini ni mji upi hasa alikuwa anauzungumza lakini wapo wataalamu wa mambokale wanaodhani huo ni mji uliokuwa katika eneo la Delta ya Rufiji.
Kilwa, Laetoli, Zanzibar, Unyanyembe na maeneo mengine ambayo sasa ni sehemu ya Tanzania yalikuwapo kabla ya mwaka 1964 na kabla ya mwaka 1920 lakini hiki kitu ambacho sasa kinajulikana kama Tanzania hakikuwepo.
Watanzania na Utanzania wao. Upole wao kwa wanadamu wengine na ukali wao dhidi ya maovu. Amani na utulivu wao, silka na tabia zao, lugha yao na vitu vingine kadhaa vimekuja kutambulika katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
Tanzania
ni muungano wa nchi mbili; Tanganyika na Zanzibar. Nchi hizi mbili
ziliungana rasmi mnamo Aprili 26, mwaka 1964 na kutengeneza jina hilo
moja. Historia inamtaja Mzee Mohamed Ikbar Dar - wakati huo akiwa
mwanafunzi wa sekondari kama mtu aliyetunga jina hilo.
Alichofanya ni kuchukua herufi tatu za mwanzo za majina ya nchi zilizoungana - Tan na Zan, na kisha; kwa maneno yake mwenyewe, kuongeza herufi mbili za IA ambacho ni ufupisho wa jina lake la kwanza na la dini yake ya Ahmaddiya. Ilisadifu pia, wakati huo, kwamba ilikuwa ni kama fasheni kwa nchi huru za Afrika kuwa na herufu hizo mbili za IA kwenye majina yake. Mfano ni nchi kama Somalia, Nigeria, Tunisia, Algeria na Ethiopia.
Hilo
ndilo jina lililopitishwa na kukubaliwa na leo nchi inajulikana hivyo
na watu wake wakiitwa Tanzania. Isingekuwa ubunifu huo wa Ikbar, pengine
nchi hii ingekuwa sasa inajulikana kwa jina lingine - watu wengi
walikuwa wakitarajia pengine nchi ingeitwa Azania.
Jina
la Tanganyika ni mchanganyiko wa majina mawili pia; Tanga - ikimaanisha
kutembea au kuzunguka (kutangatanga) na nyika ambao ni uwanda wa pori.
Zanzibar yenyewe imetokana na neon Zenj - ikimaanisha watu weusi ambao
ndiyo walikuwa wenyeji waliokutwa na wageni kutoka ng'ambo waliokwenda
kutembelea visiwa hivyo.
Pasipo
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kusingekuwa na nchi inaitwa
Tanzania leo. Wakati Muungano huo ukitokea, dunia ilikuwa katika wimbi
la Vita Baridi na Zanzibar ikitazamwa kwa jicho la kipekee kama nchi
inayoweza kugeuka kuwa 'Cuba' ya Afrika.
Vitabu
na maandishi kadhaa vilivyowahi kuandikwa kuhusu Muungano vinaeleza
kuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alikubali Muungano
kwa sababu pia alitaka kuwa na swahiba wa kisiasa - nchi, kumsaidia
kupambana na aliowahisi kuwa washindani wake wa kisiasa katika siku za
awali za utawala wake.
Mambo
mengi ni ya kufikirika zaidi lakini pasipo Muungano, huenda siasa za
Zanzibar zisingekuwa zilivyo sasa na kama siasa za visiwani
zingebadilika, ni wazi kwamba na siasa za Tanganyika zisingebaki kama
zilivyo. Pasi na shaka yoyote, Tanzania ya leo ingekuwa tofauti na
ambayo ingetokea.
Kama
hatimaye mahasimu wa kisiasa wa Karume wangefanikiwa kumtoa madarakani -
na kwa namna walivyokuwa na mtazamo wa kimajumui, ni wazi Tanganyika
ndiyo ingekuwa lengo lao la pili. Pasi na shaka yoyote, historia ya
Tanzania ya leo isingekuwa hii ilivyo sasa.
Miongoni mwa nguzo muhimu za amani na utulivu wa Tanzania ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Katika mojawapo ya siku za giza kabisa kwenye historia ya taifa hilo ilikuwa ni Januari mwaka 1964 wakati baadhi ya askari walipotaka kuasi. Kama jaribio lile lingefanikiwa, huenda historia ya Tanzania ingekuwa tofauti.
Jaribio lile lilizimwa na ndilo lililomfanya aliyekuwa Rais wa Tanganyika wakati ule, Julius Nyerere, kuamua kulivunja lililokuwa Jeshi la KAR na kuunda JWTZ. Kwa namna lilivyosukwa na kujengewa itikadi, jeshi hilo liliiepusha Tanzania na rabsha za wanajeshi ambazo zilikuwa jambo la kawaida katika nchi nyingi za Kiafrika.
Kwamba Tanzania imekuwa mojawapo ya mataifa machache ambayo hayajawahi kushuhudia mapinduzi ya kijeshi ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya kuundwa kwa JWTZ lakini kutokana na kushindwa kwa uasi wa wanajeshi wa mwaka 1964.
Tanzania ni mojawapo ya mataifa machache ya Kiafrika ambayo yanaunganishwa na lugha moja isiyo ya kigeni. Hii ndiyo imekuwa lugha isiyo na kabila, dini, ukanda wala kipato. Watanzania, karibu wa makundi yote, wanazungumza lugha moja ya Kiswahili.
Lugha hii ambayo ina ushawishi mkubwa wa lugha za kibantu na kiarabu, ina tabia zake ambazo zina utu, uungwana na upendo. Ndiyo sababu, kumekuwa na utani katika baadhi ya nchi jirani na Tanzania kwamba raia wake ni watu "wanaoomba" hata kwa vitu ambavyo wanavinunua kwa fedha zao.
Lugha
hii moja imesaidia sana kuunganisha nchi ambayo ina makabila zaidi ya
120 yenye mila, desturi na tamaduni zake tofauti. Kama isingekuwa
jitihada za makusudi za kukifanya Kiswahili kiwe Lugha ya Taifa, huenda
leo kungekuwa na matatizo mengine ambayo yanazikuta nchi nyingine.
Mathalani,
ukabila hautajwi kuwa tatizo nchini Tanzania, asili yake inaweza kuwa
inatokana na watu wote kuweza kuwasiliana kwa kutumia lugha moja ambayo
inaonekana kuwa ni ya wote, ingawa wenyeji watasema ni ya watu wa pwan
Kwa
namna moja au nyingine, kama kuna mtu mmoja anaweza kusema ana mkono
muhimu zaidi katika uumbaji wa Tanzania, basi mtu huyo ni Baba wa Taifa,
Julius Nyerere. Kuliko mtu mwingine yeyote au taasisi nyingine yoyote,
amehusika katika kuifanya Tanzania iwe ilivyo leo.
Tofauti
na Ulaya au Asia ambako nchi zilijengwa kwa misingi ya kujikinga na
vita au kwenda vitani, nchi za Afrika ziliundwa kutokana na mapatano ya
mkutano wa Berlin wa Novemba 1884 hadi Februari 1885. Hata nchi yenyewe
ya Tanganyika iliundwa na Jumuiya ya Mataifa (League of Nations) baada
ya Vita vya Kwanza vya Dunia wakati taifa hilo lilipogawiwa kwa
Uingereza kutoka kwa Ujerumani.
Kwa
hiyo, wakati Nyerere anakabidhiwa nchi na Waingereza mwaka 1961, hakuwa
na hofu ya kuingiliwa kwenye mipaka yake wala kwenda kuvamia nchi
nyingine kwa sababu jambo hilo tayari lilishakatazwa kwenye sheria za
kimataifa.
Yeye
ndiye alijenga mfumo wa kisiasa unaowapa viongozi mamlaka kuliko raia
wao. Pengine, mfumo huu ndiyo ambao umesababisha aina ya siasa zilizoko
Tanzania ambako wananchi - kwa muda mrefu, ni kama hawakuwa na habari
sana na masuala ya uwajibikaji wa viongozi wao.
Yeye
ndiye aliyeunda JWTZ na Chama Cha Mapinduzi (CCM) - taasisi mbili
ambazo zimekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania. Ni yeye
pia aliyekuwa mchagizaji mkuu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili na
mwendeshaji wa siasa ya nje ya taifa lake.
Chama cha Mapinduzi - CCM
Zaidi
ya asilimia 70 ya Watanzania hawajawahi kuona chama kingine cha sasa
kikiwa madarakani mbali na CCM katika uhai wao. Hiki ndicho chama
ambacho kwa takribani miaka 50 kimeongoza nchi kwa kutumia sera na
miongozo.
Kwa sababu hiyo, kiwango cha kuendelea (kutoendelea), kilichopo Tanzania sasa, kina uhusiano wa moja kwa moja na chama ambacho kimekuwa madarakani kwa muda wote wa uhai wa taifa hili.
CCM ndiyo imetoa mwongozo wa nchi kwenye maeneo kama elimu, afya, miundombinu, uchumi, siasa na masuala mengine muhimu kwa taifa. Pasi na shaka yoyote, kama chama cha Zuberi Mtemvu ndiyo kingeingia madarakani baada ya Uhuru na siasa zake za "Afrika kwa Waafrika" pengine Tanzania ingekuwa tofauti na ilivyo sasa.
Barani Afrika, kuna nchi chache zinaweza kusema kwamba zina chama kimoja cha siasa chenye ushawishi wa aina ambayo CCM imekuwa nayo kwa Tanzania na Watanzania kwa ujumla.
Vita vya Kagera
Taifa
lolote hujengwa kwa matukio ambayo huibua mashujaa watakaozungumzwa
vizazi na vizazi. Katika miaka yake 60, Tanzania ilipigana katika vita
moja dhidi ya Uganda ambapo iliibuka mshindi kwa kuondoa madarakani
utawala wa Nduli Idi Amini Dada.
Julius
Nyerere akaweka rekodi ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu pekee aliyeipeleka
Tanzania vitani na kuibuka mshindi - lakini tukio hilo likitengeneza
historia ya kudumu ya watu kama Jenerali Abdallah Twalipo, Jenerali
David Musuguri, Jenerali Ernest Mwita Kiaro, Luten Jenerali Silas
Mayunga, (Mti Mkavu), Luteni Jenerali Tumaini Kiwelu, Brigedia John
Butler Warden, Brigedia Benjamin Msuya na wengine wengi walioshiriki
vita hiyo.
Jambo
kubwa kuhusu vita ile ni kwamba Watanzania - sasa wakiwa nchi huru,
waliungana kwa pamoja vitani na kukubali kuifia nchi yao kwa sababu ya
bendera yao na si ya mkoloni.
Matukio
ya kukusanya watu, kuchangia mali na damu, kusafirisha watu na nyimbo
za kimapinduzi zilizoimbwa na wasanii mbalimbali zilisaidia sana katika
kujenga Tanzania ya wakati ule na msingi wake ungalipo hadi leo.
Simba na Yanga
Ukitaka
kujua vilabu hivi viwili vya mchezo wa soka vina maana gani kwa
Tanzania, inabidi nitoe mfano mmoja ninaoujua. Mmoja wa marais wastaafu
wa Tanzania alipata kuniambia kwamba hakuna namna ambayo tarehe ya
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania inaweza kupangwa katika siku ambayo kuna
pambano la Watani wa Jadi.
Inajulikana kwamba wakati Simba na Yanga zinapocheza, Tanzania karibu yote husimama. Kuliko chama cha siasa au dini nyingine yoyote, hakuna taasisi inayoweza kujidai kuwa na ufuasi ambao vilabu hivi vinao. Vilabu hivi vinakusanya masikini na matajiri, vijana na wazee, wanawake na wanaume, watu wa rangi, dini na makabila yote wanashabikia timu hizi.
Timu
hizi mbili zimeshiriki katika kujenga umoja na amani miongoni mwa
Watanzania. Kwenye kushabikia timu hizi mbili, hakuna ubaguzi au tofauti
ya aina yoyote na wala hakuna klabu mojawapo ya hizo inayoweza
kufungamanishwa na dini, dhehebu au chama chochote cha siasa.
Misri
wanajivunia vilabu vya Al Ahly na Zamalek lakini kuna itikadi za kidini
au siasa ambazo unaweza kuziunganisha na vilabu hivyo viwili - jambo
ambalo ni tofauti na Simba na Yanga ambazo ziko kwenye miji yote, dini
zote, vyama vyote na miongoni mwa watu wa rangi zote.
Kwa hiyo, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wanaweza kuwa na itikadi tofauti kisiasa lakini kwenye Yanga wanakuwa kitu kimoja. Inawezekana Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wanapishana kisiasa lakini linapokuja suala la Simba, wanakuwa kitu kimoja.
Si
sawa na Kenya ambako Gor Mahia inahusishwa moja kwa moja na watu wa
kabila la Wajaluo au AFC Leopards na kabila la Waluhya. Taasisi hizi
mbili - ni miongoni mwa nguzo kubwa ya ndoto ile inayoitwa Tanzania.
Watu na matukio niliyoyataja, yamesaidia sana katika kutengeneza taifa la Tanzania kwa namna linavyoonekana sasa kwa ndani na nje ya mipaka yake. Hata hivyo, ujenzi wa taifa ni suala endelevu na pasi na shaka yoyote bado kuna sura (chapters) nyingine bado hazijafikiwa wakati wake au kusomwa kupitia makala hii.
Hata
hivyo, katika kipindi hiki cha miaka 60 iliyopita, unaweza kusema
kwamba pamoja na mapungufu mengine yaliyopo katika nyanja kama vile
uchumi, haki za kiraia, afya, elimu na kwingineko, angalau waasisi
wamefanikiwa kujenga utaifa wa Tanzania ingawa kazi hiyo bado
haijakamilika.