SERIKALI ya Jubilee inaendelea kuongezea Wakenya mzigo wa madeni muda wake wa kwenda nyumbani unapokaribia kwa kukopa Sh300 bilioni zaidi kati ya Januari na Mei 2022.
Hii imefikisha deni la kitaifa hadi Sh8.5 trilioni.
Takwimu kutoka Hazina ya Kitaifa zinaonyesha kuwa Kenya iliendelea kukopa kutoka kwa mashirika ya kifedha ya humu nchini na yale ya kigeni ndani ya kipindi hicho hadi kiwango cha asilimia 69.1 cha utajiri wa nchini kutoka asilimia 66.7 mnamo Januari.
Kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Amerika pia kumechangia kuongezeka kwa gharama ya ulipaji wa madeni hayo katika mwaka huu wa kifedha wa 2021/2022 ulioanza Julai 1.
Thamani ya shilingi ya Kenya ilidorora kwa kiwango cha asilimia 0.8 katika kipindi hicho, kutoka Sh115 kwa dola moja mnamo Januari hadi Sh117 mwezi Mei.
“Kwa jumla, serikali ya kitaifa ilikopa Sh51.57 bilioni zaidi kutoka nje kuanzia Januari mwaka huu na kuongezea deni la Sh4.24 trilioni ambalo Kenya ilikuwa ikidaiwa kufikia Aprili 2022,” ikasema Hazina ya Kitaifa.
Hii ina maana kwamba serikali ilikopa jumla ya Sh242.5 bilioni kutoka kwa mashirika ya kifedha ya humu nchini.
Tayari kufikia Mei Serikali imepitisha kiwango cha fedha ambacho ilipaswa kukopeshwa kutoka humu nchini kufikia Juni, 2022, hali inayowaongezea walipa ushuru mzigo zaidi. Hii ni kwa sababu madeni kutoka humu nchini hutozwa kiwango cha juu cha riba.
Kwa jumla, kiwango cha fedha ambazo serikali ilipaswa kulipa kama riba kwa madeni iliyokopa kutoka mashiriki ya kifedha humu nchini kilifikia Sh427.25 bilioni kufikia Mei 2022.