Wabunge wa chama cha tawala nchini Uingereza cha Conservative watapiga kura leo katika duru ya pili ya mchujo wa wagombea wanaowania kumrithi waziri mkuu Boris Johnson aliyetangaza kujiuzulu wiki moja iliyopita. Katika duru ya kwanza iliyofanyika jana waziri wa zamani wa fedha Rishi Sunak aliwapiku wanasiasa wengine kadhaa kwa kujipatia kura 88 na kujisafishia njia kama mgombea anayeweza kutoa ushandani mkali kwenye kinyang´anyiro cha kumrithi Johnson. Wagombea wengine waliofanya vizuri wakati wa kura hiyo ya mchujo ni naibu waziri wa biashara Penny Mordaunt aliyepigiwa kura 67 na waziri wa sasa wa mambo ya kigeni Liz Truss aliyeambulia kura za wabunge 50. Akizungumza kuelekea kura ya leo Rishi Sunak amesema iwapo atakuwa waziri mkuu kipaumbele chake cha kwanza kiuchumi itakuwa ni kushughulikia mfumuko mkubwa wa bei badala ya kupunguza kodi kama baadhi ya wagombea wengine walivyoahidi.