YAMKUTA HAYA MUWANIA KITI CHA URAIS KENYA

KINYANG’ANYIRO cha kiti cha urais kimekumbwa na hali ya suitofahamu baada ya kuwasilishwa kwa kesi ya kumtimua mwaniaji urais wa chama cha Roots Profesa George Wajackoyah kwa madai kwamba yeye ni hatari kwa usalama kwa vijana na fisi.

Mahakama kuu inaombwa ifutilie mbali uwaniaji wa Prof Wajackoyah kwa vile anahimiza ukuzaji na uuzaji wa bhangi,kuuzwa kwa nyeti za fisi, kuuzwa kwa sumu na nyama za majoka ng’ambo Uchina kulipa deni la trilioni tisa inayodaiwa nchi hii na Uchina na mataifa mengine..

Katika kesi aliyowasilishwa Ijumaa katika Mahakama kuu, wakili Bernard Odero Okello, anaomba tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ifutilie mbali uteuzi wa Prof Wajackoyah kuwania urais.

Bw Okello anaomba mahakama kuu iamuru Prof Wajackoyah apimwe kubaini utimamu wa akili yake kutokana na matamshi yake katika midahalo ya umma.

Wakili huyo anaomba mahakama kuu itangaze Prof Wajackoyah hafai kuhudumu katika wadhifa wa urais kutokana na matamshi yake kwamba “atasitisha kutumika kwa Katiba iliyozinduliwa na kupitishwa 2010.”

Mbali na kutangaza Prof Wajackoyah hafai kuwania urais, Bw Okello, amesema nia ya mwaniaji huyo wa urais sio nzuri kwa vile ametangaza ataamuru kunyongwa kwa washukiwa wa ufisadi kwa kutiwa kitanzi na kuamuru raia wa kigeni wasiofanya kazi warudishwe makwao.

Pia anasema Prof Wajackoyah atafutilia mbali Katiba kisha azindue utawala wa udikteta.

Akili timamu

Kwa mujibu wa sheria, Bw Okello anasema mwaniaji wa kiti cha urais anatakiwa kuwa raia wa Kenya, aliyekomaa na mwenye akili timamu.

Pia anatakiwa kuwa mwaminifu kwa nchi yake asiyekuwa na imani na nchi nyingine.

Bw Okello anasema mwaniaji kiti cha urais anatakiwa kutimiza sheria na masharti yaliyowekwa kabla ya kuteuliwa kuwania urais.

Alipoidhinishwa kuwania urais na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Prof Wajackoyah alitangaza manifesto yake mnamo Juni 30 ,2022 na kuweka wazi wazi kwamba:- atahalalisha ukuzaji na uuzaji wa bangi, ataruhusu ufugaji wa majoka, kuuza ng’ambo nyama ya mbwa, kufunga reli ya kisasa (SGR), kuhamisha jiji kuu la Kenya kutoka Nairobi hadi Isiolo, kubuni majimbo manane badala ya kaunti 47 zilizopo sasa, watu kufanya kazi siku nne kwa wiki na kuwarudisha makwao raia wa kigeni wasio na kazi.

Wakili huyu amedai Prof Wajackoyah alieleza vyombo vya habari yuko na uraia wa Uingereza na kwamba wakati mmoja aliwania kiti cha Ubunge cha Totten Ham Uingereza.

Matamshi hayo, Bw Okello anasema yanatilia shaka uaminifu wake Prof Wajackoyah kwa nchi hii.

Pia mahakama imeelezwa kuwa msimamo huo wa Prof Wajackoyah na mwashirio wake katika masuala anayoshambikia unatilia shaka utimamu wa akili yake.

Wakili huyo anaomba mahakama kuu iamuru Prof Wajackoyah pamoja na wawaniaji wengine wapimwe akili.

Bw Okello anaomba mahakama kuu ishutumu IEBC kwa kukaidi sheria kwa kuamuru wawaniaji wa kiti cha urais wapimwe utimamu wa akili zao.

Pia anaomba agizo wawaniaji wa kiti cha Urais wawe wakipimwa akili kabla ya kuteuliwa kuwania urais.

Bw Okello anasema Mahakama kuu iko na uwezo wa kusikiza na kutoa maagizo anayoomba chini ya Vifungu nambari 23 na 165 vya Katiba.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii