MASAIBU yanayomkumba Gavana Granton Samboja yameibuka upya, baada ya mpigakura kujaribu tena kumzuia kutetea kiti hicho katika uchaguzi unaopangiwa kufanyika Agosti.
Bw Jeremiah Kiwoi, ameenda kortini kutaka mahakama iagize Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutomwidhinisha gavana huyo kutetea wadhifa huo.
Kesi hiyo imewasilishwa siku chache baada ya Bw Samboja kupata afueni, wakati jopo la IEBC lilitupa nje ombi lingine lililotaka azuiwe kuwania ugavana.
Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa katika Mahakama ya Kikatiba na Haki za Kibinadamu jijini Nairobi, Bw Kiwoi anadai gavana huyo hastahili kuwania wadhifa ya uongozi kwa madai kuwa alifeli katika uadilifu baada ya kughushi cheti cha digrii mnamo 2017.
Kupitia wakili wake, Bw Manase Mwangi, mlalamishi huyo anadai gavana aliunda cheti feki alipokuwa anawania kiti hicho 2017 na hivyo kuihadaa kaunti hiyo.
“Ikiwa mahakama haitaingilia kati, uovu huu utaendelea na kuwasababisha madhara wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta,” akasema.
Alisema licha ya kuwa aliwasilisha maombi ya kumzuia gavana huyo kwa kamati ya IEBC, jopo lilitupilia mbali kesi hiyo.
“Licha ya kuwa na ushahidi wa kutosha, kamati hiyo ilitupilia mbali ombi hilo na hivyo kukiuka haki zangu za kupata haki ya uamuzi wa kesi hiyo,” akasema.
Vile vile, alisema gavana huyo alitoa maelezo yasiyo ya ukweli kwa IEBC na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kupitia fomu ya kujitangaza aliyowasilisha kwa tume hizo.
“Chuo cha Kenyatta kilisema gavana hakuhitimu na shahada ya Biashara na hivyo vyeti vyake vilikuwa ghushi. Aidha, katika fomu ya kujitangaza aliyowasilisha kwa IEBC na EACC, gavana huyo alisema hajawahi kutoa maelezo yasiyo ya ukweli,” akasema.
Stakabadhi zilizotumiwa na Bw Samboja kupata cheti cha IEBC zilionyesha kuwa, alisomea shahada ya Biashara katika Chuo cha Costa Rica kinyume na 2017 alipodai kuwa alisomea chuo cha Kenyatta.
Tangu maandalizi ya uchaguzi ujao yalipoanza kushika kasi, mpigakura huyo ambaye pia ni mwenyeji wa kaunti hiyo amekuwa akijaribu kumzuia Gavana Samboja kutetea kiti hicho katika uchaguzi ujao bila mafanikio.
Mnamo Mei, Bw Kiwoi alikitaka Chama cha Jubilee kutompa tikiti ya kuwania kiti hicho na kukitaka kichunguze iwapo Bw Samboja alikuwa na vyeti halisi kwanza.