SERIKALI Kuu sasa imepata idhini ya kuchukua mkopo wa hadi Sh10 trilioni kutoka Sh9 trilioni baada ya maseneta kupitisha pendekezo la Wizara ya Fedha kuhusu suala hilo.
Jumla ya maseneta 27 walipiga kura ya NDIO na watatu wakapiga kura ya LA katika shughuli iliyoondeshwa katika ukumbi wa seneti Jumanne jioni.
Wale waliopinga pendekezo la kuongezwa kwa kiwango cha mkopo ni Seneta wa Nandi Samson Cherargei, Aaron Cheruiyot (Kericho) na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.
Pendekezo hilo la kuongezwa kwa kiwango cha fedha ambazo serikali inaweza kukopa lilipitishwa katika bunge la kitaifa mnamo Juni 9, 2022 wabunge walipoahirisha vikao vyao ili kutoa nafasi wao kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Kuongezwa kwa mkopo hadi Sh10 trilioni kutaiwezesha serikali kuziba pengo kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha za 2022/2023 ambalo ni Sh846 bilioni.
Bajeti hiyo ya kima cha Sh3.3 trilioni ilisomwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani katika bunge la kitaifa mnamo Aprili 7, 2022.
Wakati huu serikali inakabiliwa na mzigo wa madeni wa Sh8.4 trilioni.
Hoja ya kupandisha kiwango cha madeni hadi Sh10 trilioni iliungwa mkono na wabunge wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya wakiongozwa na kiongozi wa wengi Amos Kimunya.
Wabunge hao walifanya hivyo kwa kuifanyia marekebisho Kanuni ya Usimamizi wa Fedha za Umma katika Serikali ya Kitaifa ya 2015.
Kanuni hiyo ilichapishwa kama notisi ya kisheria ya 89 ya 2022.
“Kwa mujibu wa hitaji la Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM act), Bunge hili linapitisha Kanuni ya Sheria hiyo ya 2022, kwa kuamuru kwamba deni la kitaifa halitazidi Sh10 trilioni,” hoja hiyo maalum ikasema.
Serikali ijayo itatarajiwa kutekeleza bajeti hiyo ya kima cha Sh3.3 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2022/23 inayoanza Julai 1, 2022. Bajeti hiyo ina pengo la Sh846 bilioni ambalo serikali inafaa kuliziba kwa kukopa humu nchini na nje.
Wabunge wengine waliunga mkono hoja hiyo ni pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kanini Kega, Opiyo Wandayi (Ugunja), William Kamket (Tiaty) na Jeremiah Kioni (Ndaragua).