Wanawake wa Kiislamu nchini India wapinga ndoa za wake wengi

Hatua ya mwanamke wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 28 ya kuomba mahakama nchini India kumzuia mme wake kuoa mke mwingine bila ya ridhaa yake ya maandishi kumezua mjadala wa wazi kuhusu mila ya ndoa za mitala miongoni mwa Waislamu nchini humo.

Reshma, ambaye anatumia jina moja pekee, pia anataka Mahakama Kuu ya Delhi kuamuru serikali kutunga sheria za kudhibiti "mila ya kurudisha nyuma" ya upendeleo au mitala.

Kulingana na hati ya mahakama, alifunga ndoa na Md Shoeb Khan Januari 2019 na Novemba mwaka uliofuata, wanandoa hao walipata mtoto.

Reshma anamshutumu mumewe kwa unyanyasaji wa nyumbani, ukatili, unyanyasaji na madai ya mahari. Ametoa tuhuma kama hizo dhidi yake.

Pia anasema kuwa amemtelekeza yeye na mtoto wao na ana mpango wa kuoa mke mwingine.

Akielezea kitendo chake kama "kinyume cha katiba, kinyume cha sharia, kinyume cha sheria, kitendo cha kikatili na kinyama", anasema "tabia hii inahitaji kudhibitiwa ili kupunguza masaibu ya wanawake wa Kiislamu".

Wakati mahakama ikizingatia uhusiano wao wa chuki na uhalali wa mitala, kesi hiyo imezua mjadala juu ya mila hiyo ambayo si halali nchini India isipokuwa kwa miongoni mwa Waislamu na baadhi ya jamii za makabila.

Takriban 2% ya watu duniani wanaishi katika kaya zenye wake wengi, kulingana na ripoti ya Kituo cha Utafiti cha Pew 2019. Kitendo hicho kimepigwa marufuku katika sehemu kubwa ya dunia, ikiwa ni pamoja na katika nchi za Kiislamu kama vile Tunisia, na kimedhibitiwa katika nchi nyingi ambazo zinaruhusu utaratibu huo. Umoja wa Mataifa umetaja kama "ubaguzi usiokubalika dhidi ya wanawake" na kutoa wito "ukomeshwe kabisa".

Lakini nchini India, suala hili limezua moto kisiasa. Chama cha Bharatiya Janata (BJP) cha Waziri Mkuu Narendra Modi kimeahidi kutunga Kanuni ya Kiraia (UCC) - kifungu cha sheria chenye utata ambacho kitamaanisha ndoa, talaka na urithi havitatawaliwa tena na sheria zao za kidini bali vitakuwa chini ya sheria ya kawaida inayotumika kwa raia wote.

Na katika wakati ambapo nchi ina mgawanyiko mkubwa katika misingi ya kidini, mageuzi yoyote yanayopendekezwa na serikali ni lazima yachukuliwe kuwa ni mashambulizi dhidi ya Uislamu na Waislamu walio wengi.

SY Qureshi, kamishna mkuu wa zamani wa uchaguzi na mwanazuoni wa Uislamu, anasema nchini India, "mtazamo wa jumla ni kwamba kila Mwislamu ana wake wanne" na kwamba wana watoto wengi ambao hatimaye itawafanya Waislamu kuwazidi Wahindu, lakini hiyo si kweli. (Ni 14% tu ya watu bilioni 1.3 wa India ndio Waislamu wakati Wahindu ni 80% ya idadi ya watu.)

Wanaume Waislamu nchini India wanaruhusiwa kuoa hadi wanawake wanne na idhini ya mitala, anasema, inatoka katika Qur'an, lakini inaruhusiwa tu chini ya "masharti na vikwazo vikali" ambavyo ni vigumu sana kutimizwa.

"Qur'an inasema mtu anaweza kuoa mke wa pili au wa tatu au wa nne lakini tu kutoka kwa mayatima na wajane na kwamba lazima awatendee wote sawa tofauti na hapo ni ukiukwaji. Lakini kupenda wote kwa usawa ni kitu ambacho hakiwezekani na sio suala la kuwanunulia nguo sawa, ni zaidi ya hayo," anaongeza.

Mwongozo kuhusu mitala, Bw Qureshi anasema, ulijumuishwa katika Kurani katika Karne ya 7 huku kukiwa na vita vya kikabila huko Uarabuni wakati wanaume wengi walikufa wakiwa wachanga na mitala ilikusudiwa kuwasaidia wajane na mayatima. "Vinginevyo, Quran kwa hakika haimasishi tabia hiyo na inaidharau."

Wakosoaji kama vile mwanaharakati wa haki za wanawake Zakia Soman wanasema kwamba leo hakuna vita nchini India na ndoa za wake wengi - "mila potofu na ya mfumo dume" - lazima ipigwe marufuku.

Mwanzilishi wa Bharatiya Muslim Mahila Andolan (BMMA - Indian Muslim Women's Movement) yenye makao yake Mumbai, Bi Soman anasema ndoa za wake wengi "ni chukizo - kimaadili, kijamii na kisheria" na ukweli kwamba "kuruhusiwa kisheria inafanya kuwa na matatizo".

"Unawezaje kusema kuwa mwanaume mmoja anaweza kuwa na wake zaidi ya mmoja? Jamii inabidi iende mbele na wakati. Katika zama hizi ni ukiukwaji mkubwa wa utu na haki za binadamu."

Mnamo mwaka wa 2017, BMMA ilichunguza wanawake 289 waliokuwa na uhusiano wa wake wengi na kuwauliza kuhusu hali yao ya kimwili, kiakili, kihisia na kifedha. Wametoa ripoti inayoelezea kesi 50.

"Tuligundua kwamba walikuwa katika hali ambazo hazikuwa za haki kwa wote, ilikuwa uzoefu wa kutisha na wengi walikuwa na matatizo ya afya ya akili," Bi Soman anasema.

BMMA, ambayo hapo awali ilikuwa imefanya kampeni kubwa dhidi ya mila yenye utata ya talaka ya papo hapo katika Uislamu hadi ilipopigwa marufuku miaka michache nyuma, iliwasilisha ombi kwa Mahakama ya Juu mwaka 2019, ikitaka kupigwa marufuku kwa mitala.

Kuna changamoto nyingine za kisheria pia ikiwemo ile ya Ashwini Kumar Dubey, wakili na kiongozi wa chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) cha India.

Hii imesababisha shutuma kutoka kwa Waislamu wa kihafidhina kwamba ni kuingilia dini yao.

"Katika Uislamu, sheria ni za Kimungu, tunazingatia Qur'an na Hadith kwa maelekezo. Hakuna mwanadamu mwenye haki ya kubadilisha kile kilichohalalishwa na Mwenyezi Mungu," anasema Dk Asma Zohra, All India Muslim Personal Law Board (AIMPLB) ambayo inapinga ombi la Bw Dubey mahakamani.


Ndoa za wake wengi miongoni mwa Waislamu, anasema, "ni nadra na sio tatizo" na anashutumu BJP kwa kufanya ni ajenda ya watu wachache kuwaamulia watu wnegi.

"Je, umewahi kukutana na mwanamume Mwislamu ambaye ana wake wanne? Katika mwaka wa 2022, wanaume wengi wanasema ni vigumu kutunza mke mmoja, acha peke yake kutunza wanne. Na kiwango cha ndoa za mitala ni kidogo zaidi katika jamii ya Kiislamu."

Madai yake yanatokana na data ambayo iligundua ndoa za wake wengi zimeenea miongoni mwa dini zote - utafiti kulingana na sampuli ya ukubwa wa ndoa 100,000 na Sensa ya India mwaka 1961 ulionyesha mitala miongoni mwa Waislamu kuwa 5.7%, ambayo ni ya chini zaidi kati ya jamii zote.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii