Boti ya wahamiaji yazama Senegal watu 21 wafariki

Watu wasiopungua 21 wamefariki dunia baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji kuzama katika Bahari ya Atlantiki, karibu na Kébémer, kaskazini-magharibi mwa Senegal, takriban kilomita 180 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Dakar.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Senegal ilisema hadi Jumamosi jioni, Novemba 7, waokoaji walikuwa wameopoa miili ya watu 21 na kufanikiwa kumwokoa mtu mmoja.

Wizara hiyo ilieleza kuwa idadi hiyo ni ya awali huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea. Hata hivyo, haikubainisha idadi ya watu waliokuwa ndani ya boti hiyo wakati ilipozama.

Katika tukio jingine, mamlaka za Senegal zimesema ziliizuia Ijumaa boti iliyokuwa ikielekea katika Visiwa vya Kanari vya Uhispania ikiwa na wahamiaji 142 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Magharibi.

Serikali ya Senegal imesema itaongeza ushirikiano na nchi jirani katika kukabiliana na mitandao inayojihusisha na usafirishaji haramu wa wahamiaji.

Wakati huo huo, mamlaka za kisiwa cha El Hierro, mojawapo ya Visiwa vya Kanari vya Uhispania, zimetangaza hali ya dharura Ijumaa, Novemba 6, kufuatia ongezeko kubwa la wahamiaji wanaowasili kwa kutumia boti.

Kwa mujibu wa mamlaka za kisiwa hicho, zaidi ya watu 3,300 wamewasili kwa kutumia takriban boti 30 tangu mwanzoni mwa Novemba mwaka huu.

Mkuu wa Baraza la El Hierro, Alpidio Armas, aliiambia televisheni ya umma ya Uhispania kuwa hatua hiyo inalenga kurahisisha uratibu na kuwezesha upatikanaji wa msaada zaidi kutoka kwa serikali ya eneo la Kanari na serikali kuu ya Uhispania.

Alisema ongezeko hilo limeongeza shinikizo kwa huduma muhimu za kisiwa hicho, ikiwemo hospitali, huku El Hierro ikiwa na wakazi wapatao 11,400.

Katika miaka ya karibuni, maelfu ya watu wamepoteza maisha wakijaribu kuvuka Bahari ya Atlantiki kutoka Afrika Magharibi kuelekea Visiwa vya Kanari.

Mwaka 2024, idadi ya wahamiaji waliofika katika visiwa hivyo ilifikia rekodi ya takriban 46,000. Idadi hiyo ilipungua baada ya kuimarishwa kwa doria na ushirikiano kati ya Uhispania na mataifa ya Afrika, kabla ya kurekodiwa tena kwa ongezeko la wahamiaji mwanzoni mwa Novemba mwaka huu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii