BoT YAWEKA NJIA RAHISI KWA WANANCHI KUPATA HAKI WANAPODHULUMIWA NA WATOA HUDUMA ZA FEDHA

WANANCHI wanaotumia huduma za kifedha nchini sasa wanaongezewa fursa ya kuwasilisha malalamiko na kufuatilia utatuzi wake kwa urahisi kupitia mfumo wa kidijitali wa Sema na BoT, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa watumiaji na kuwapa nafasi ya kudai haki zao wanapokabiliana na changamoto.

Mfumo huo uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za malalamiko, kuongeza uwazi na ufanisi katika kushughulikia changamoto zinazotokana na huduma za kifedha zinazotolewa na benki pamoja na taasisi nyingine za fedha zilizopewa leseni.

Akizungumza Novemba 5, 2026, jijini Dar es Salaam, Afisa Benki Kuu kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha Janeth Kiwia, amesema mfumo huo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watumiaji wa huduma za kifedha wanalindwa na wanapata haki zao wanapokumbana na huduma zisizoridhisha.

Amesema BoT ina jukumu la kusimamia namna taasisi za fedha zinavyopokea, kushughulikia na kutatua malalamiko ya wateja, ili kuhakikisha hakuna mtumiaji anayekosa haki yake kutokana na kukosa njia ya kufikisha changamoto anazokutana nazo.

Ameeleza kuwa usimamizi huo unazingatia sheria na miongozo ya mwaka 2019 na 2025, inayozitaka taasisi za fedha kuwa na mifumo madhubuti ya kupokea na kutatua malalamiko kupitia njia mbalimbali ikiwemo simu, barua pepe, barua za kawaida na madawati ya huduma kwa wateja.

Kiwia alikuwa akizungumza wakati wa semina ya siku tatu iliyoandaliwa na BoT kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha nchini, akieleza namna Benki Kuu inavyotumia mfumo wa Sema na BoT kuimarisha ulinzi wa watumiaji na kuongeza ufanisi katika utatuzi wa malalamiko yanayotokana na huduma za kifedha. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii