Vitongoji 1,597 kati ya 3,448 vilivyopo mkoani Mwanza vimefikishiwa umeme, huku kazi ya kusambaza huduma hiyo ikiendelea katika vitongoji vingine 619 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage, wakati akielezea maendeleo ya miradi ya umeme inayotekelezwa na REA mkoani Mwanza.
Amesema mkoa huo tayari umefikishiwa umeme katika vijiji vyote, na kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kusambaza huduma hiyo katika vitongoji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mwijage ameongeza kuwa REA, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeanza kutekeleza mradi wa kufikisha nishati kwa wananchi wanaoishi visiwani, kwa kutumia mifumo ya umeme wa jua inayopatikana kwa gharama ya ruzuku ya Serikali.
Amesema Serikali inatoa ruzuku ya asilimia 45 hadi 75 kwa mifumo hiyo ili kupunguza gharama kwa wananchi na kuwawezesha kupata nishati kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli za maendeleo.
Akizungumza wakati wa kikao na REA pamoja na ujumbe kutoka Benki ya Dunia uliofika ofisini kwake kabla ya ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na benki hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, amesema nishati ni kichocheo muhimu cha maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii.
Hamduni amesema upatikanaji wa nishati ya uhakika ni muhimu katika kuimarisha sekta nyingine na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea kutambua mchango wa REA katika kusambaza umeme vijijini.
Ameishukuru Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, huku akitambua pia mchango wa Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni mtaalamu wa nishati kutoka Benki ya Dunia, Rhonda Jordan, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati kwa ajili ya maendeleo.