Mwanasiasa Gadi Eisenkot amemwalika Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kufanya mazungumzo ya haraka kuhusu uwezekano wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, baada ya Netanyahu kupendekeza makubaliano ya kugawana madaraka kupitia mfumo wa kubadilishana nafasi ya waziri mkuu.
Hatua hiyo imekuja wakati Israel ikiendelea kukabiliwa na mvutano wa kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa Oktoba, ambao haukuwezesha upande wowote kupata wingi wa viti vya kuunda serikali.
Eisenkot, ambaye alipewa jukumu na Rais wa Israel, Isaac Herzog, la kuunda serikali mpya, amekuwa akifanya juhudi za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa vyama mbalimbali ili kuiondoa serikali ya Netanyahu madarakani.
Katika pendekezo lake lililotolewa kupitia mitandao ya kijamii Jumamosi usiku, Netanyahu alisema yuko tayari kuweka pembeni tofauti za kisiasa na kukubali Eisenkot kuwa waziri mkuu kwanza, huku yeye akihudumu kama naibu waziri mkuu kwa kipindi cha mwanzo.
Akijibu pendekezo hilo, Eisenkot alisema yuko tayari kufanya mazungumzo iwapo chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu kina nia ya dhati ya kuunda serikali ya umoja.
Alimwalika Netanyahu pamoja na timu yake kukutana katika Hoteli ya Dan Accadia, iliyopo Herzliya, kwa mazungumzo ya haraka.
Eisenkot alisema anataka kuona ndani ya saa 24 iwapo Likud iko tayari kushiriki katika mazungumzo ya kweli ya kuunda serikali.
Siku moja kabla ya mwaliko huo, Eisenkot alikuwa ameahidi kutangaza serikali mpya ifikapo Desemba 6, ambayo ni siku ya mwisho ya muda rasmi aliopewa, bila kutumia siku 14 za nyongeza alizokuwa na haki ya kuomba.
Hata hivyo, juhudi zake zimekuwa zikikwamishwa na tofauti za kisiasa kuhusu vyama vya Kiarabu, vyama vya kidini vya Kiorthodoksi na uwezekano wa kushirikiana na Likud.
Ijumaa, Eisenkot aliishutumu Likud kwa kuchelewesha mazungumzo ya kuunda serikali, akidai chama hicho kimeshindwa kuwasilisha mapendekezo yoyote ya msingi kwa zaidi ya wiki mbili.
Wakati huohuo, wapinzani wa Netanyahu wamekosoa pendekezo lake la kugawana nafasi ya waziri mkuu.
Kiongozi wa chama cha Joint List, Youssef Jabareen, alisema wananchi wanataka kuondolewa kwa serikali ya Netanyahu na kuundwa kwa uongozi mpya unaowakilisha Waisraeli wa Kiyahudi na Waarabu.
Naye aliyekuwa waziri mkuu wa Israel, Yair Lapid, amelitaja pendekezo la Netanyahu kuwa ni mbinu nyingine ya kisiasa ya kudanganya washirika wake.