Msando alaumu ubomoaji wa vibanda Mbezi kwa Msuguri

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amepinga ubomoaji wa vibanda vya wafanyabiashara wadogo katika eneo la Mbezi kwa Msuguri, Dar es Salaam, akitaka mazungumzo yafanyike kabla ya kuchukua hatua zinazoweza kuathiri shughuli za wananchi.

Msando amesema Serikali ina wajibu wa kulinda masilahi ya wananchi badala ya kuwanyanyasa, akisisitiza kuwa migogoro inayohusu matumizi ya maeneo ya biashara inapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo na kufuata taratibu.

Amesema vibanda vilivyobomolewa vilikuwa vya muda, hivyo TANROADS ilipaswa kukutana na wafanyabiashara na kujadili namna ya kupata suluhisho kabla ya kubomoa mali zao walizozijenga kwa gharama na nguvu zao.

Kutokana na hatua hiyo, Msando amesema hayuko tayari kufanya kazi na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, akieleza kutoridhishwa na namna ubomoaji huo ulivyotekelezwa.

Amesisitiza kuwa ubomoaji wa maeneo ya wafanyabiashara wadogo haupaswi kufanyika bila mazungumzo na wahusika, akionya kuwa hatua za aina hiyo zinaweza kusababisha migogoro kati ya Serikali na wananchi.

Kwa upande wao, wafanyabiashara walioathirika wamesema ubomoaji huo umewapotezea maeneo yao ya kujipatia kipato na kuathiri shughuli zao za kiuchumi.

Wamedai kuwa hatua hiyo haikutendeka kwa usawa, wakieleza kuwa kuna majengo ya kudumu na vituo vya mafuta vilivyojengwa kando ya barabara ambavyo, kwa madai yao, havijachukuliwa hatua.

Wafanyabiashara hao wametaka sheria na taratibu za hifadhi ya barabara zitekelezwe kwa wote bila ubaguzi, wakitaka hata majengo yaliyojengwa ndani ya mita 12 kutoka barabarani bila vibali yashughulikiwe kwa utaratibu unaofanana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii