Ethiopia imesema itajilinda dhidi ya kile inachokiita uvamizi wa kijeshi wa Eritrea, ikidai wanajeshi wameingia hadi kilomita 60 ndani ya nchi. Eritrea inasema madai hayo yanalenga kuhalalisha vita dhidi yake.
Serikali ya Ethiopia imesema itasimama kidete kujilinda dhidi ya kile imekiita uvamizi kamili wa kijeshi wa Eritrea. Katika barua iliyoandikwa na utawala wa nchi hiyo kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kuchapishwa na shirika la habari la Reuters leo Ijumaa, Adis Ababa imesema haina chaguo jingine zaidi ya kujilinda.
Msimamo huo ndi tamko la kwanza rasmi la serikali kuhusiana na ripoti za kuingia kwa wanajeshi wa Eritrea nchini Ethiopia wiki hii. Hatua hiyo imeibuwa khofu ya kutokea vita kamili kati ya majirani hao wawili katika eneo la pembe ya Afrika.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia Gedion Timothewos amesema wanajeshi wa Eritrea wamepelekwa kaskazini mwa Ethiopia na wameingia umbali wa hadi kilomita 60.Eritrea Jumatano ilisema madai ya Adis Ababa yanadhamiria kuhalalisha azma yake ya vita na nchi hiyo.