Watu wasiopungua 82 wamefariki baada ya kuporomoka kwa mgodi wa dhahabu

Watu wasiopungua 82 wamefariki baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka nchini Sudan, nchi iliyoharibiwa na vita inayofadhiliwa kwa kiasi kikubwa na tasnia ya dhahabu, chanzo ndani ya Vikosi vya Msaada wa haraka (RSF) kilisema siku ya Jumatano, Septemba 16. Baada ya kuporomoka kwa uchumi kutokana na vita, Wasudani wengi wameingia kwenye uchimbaji mdogo wa madini wa kienyeji ili kujipatia kipato.

Tangu kuanza kwa mzozo kati ya jeshi la Sudan na RSF mnamo mwezi Aprili 2023, pande zote mbili zimenufaika kutokana na rasilimali za nchi hiyo, haswa biashara ya dhahabu ya mabilioni ya dola. Katika nchi ambayo karibu watu milioni 20 sasa wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula, kulingana na Umoja wa Mataifa, vijana wengi wa kiume wamejitosa katika harakati hatari za kusaka dhahabu, hasa katika migodi ya kienyeji kama ule ulioporomoka Jumanne katika eneo la Kordofan (kusini mwa Sudan

"Idadi isiyojulikana ya watu bado wamenaswa chini ya vifusi, na shughuli za uokoaji zinaendelea kwa kutumia vifaa duni," kimesema chanzo kutoka ndani ya kikosi cha FSR kinachodhibiti eneo hilo, kwa sharti la kutotajwa jina. Chanzo hicho pia kimeripoti watu zaidi ya hamsini walijeruhiwa.

Watu wawili walionusurika walieleza jitihada zilizofanyika usiku kucha katika kujaribu kuwaokoa wafanyakazi kwenye mgodi huo wa Al-Zaraa. 'Kila mtu anafanya kazi kwa bidii ili kuondoa miili na kutafuta manusurika wanaoweza kuwepo, lakini ni vigumu. Tunahitaji vifaa vya kutosha vya kuondoa miamba na udongo,' alisema Khair al-Sayyed Jabara.

Miili ya watu 60 ilitolewa kutoka kwenye kifusi alfajiri ya Jumatano, ikifuatiwa na wengine 22 baadaye siku hiyo.

Kulingana na maafisa wa Sudan na vyanzo ndani ya sekta ya madini, karibu dhahabu yote inayotoka Sudan kupitia njia rasmi au mitandao sambamba huishia katika Falme za Kiarabu—ambazo zinashutumiwa kwa kuwapa silaha wanamgambo wa RSF. Abu Dhabi inakanusha kuhusika madai hayo, licha ya ushahidi uliotolewa katika ripoti nyingi za kimataifa.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii