Watu 60 wameuawa katika uvamizi wa wezi wa mifugo Sudan Kusini

Watu 60 wameuawa nchini Sudan Kusini, baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha, katika uvamizi wa wizi wa mifugo katika jimbo la Warrap, Katikati ya nchi hiyo.

Maafisa wa serikali wanasema, mashambulizi mawilli yalitokea katika Kaunti ya Tonj Kaskazini, juzi Alfajiri.

Kati ya watu hao 60 waliopoteza maisha ni wavamizi kumi na watano.

Mauaji haya mabaya yametokea, licha ya rais Salva Kiir, kutangaza hali ya hatari ya miezi sita katika jimbo la Warrap, kwa sababu ya kuongezeka kwa makabiliano ya kikabila yanayohusisha wizi wa mifugo.

Msemaji wa jimbo la Warrap, William Wol Mayom Bol, amesema serikali inachunguza waliohusika na mauaji hayo, na kuahidi kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha, amedokeza kuwa jeshi la serikali limetumwa katika eneo hilo kurejejsha utulivu na kulinda amani katika tukio hilo ambalo limewaacha watu zaidi ya 50 na majeraha huku 17 wakihamishwa mjini Wau kwenda kupewa matibabu.

Mbali na mauaji hayo, mamia ya mifugo imeibiwa, huku wakaazi wakilazimika kukimbilia msituni ili kuokoa maisha yao.

Mauaji haya yametokea baada ya onyo la Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), kutoa tahadhari kuhusu ongezeko la machafuko ya kikabila katika jimbo la Warrap.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii