Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi wanaomiliki silaha kuhakikisha wanazifikisha katika mamlaka husika kwa ajili ya uhakiki na kulipia ada zinazotakiwa, akionya kuwa watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Chalamila ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisisitiza kuwa wamiliki wa silaha wanapaswa kuzifikisha katika maeneo yaliyowekwa ndani ya muda uliotangazwa.
Amesema pia ndugu wa watu waliofariki dunia wakiwa wanamiliki silaha wanapaswa kufika katika mamlaka husika ili silaha hizo zihakiwe na kufanyiwa taratibu kwa mujibu wa sheria.
Aidha, ndugu wa watu waliofariki dunia wakiwa katika mchakato wa kupata umiliki wa silaha wametakiwa kufika katika mamlaka husika ili taratibu za umiliki ziweze kuendelea kisheria.
Chalamila amewataka watu wanaomiliki silaha kinyume cha taratibu kuzifikisha haraka katika mamlaka husika kabla hawajakamatwa na vyombo vya dola.
Amesema silaha hizo zinapaswa kuwasilishwa kwa ajili ya uhakiki na taratibu nyingine zinazostahili ifikapo Agosti 30, 2026.