UNICEF "Takriban watoto Milioni 20 walirubuniwa kimapenzi"

Ripoti mpya ya shirika la watoto UNICEF imesema kuwa takriban watoto milioni 20 wanaotumia mtandao katika nchi 21 walirubiniwa kimapenzi au kufanyiwa unyanyasaji wa kingono kwenye majukwaa ya kidijitali katika kipindi cha mwaka mmoja, matukio mengi yakitokana na mitandao ya kijamii.

UNICEF inakadiria kuwa mtoto mmoja kati ya watano wenye umri wa miaka 12 hadi 17 barani Afrika, Asia, Amerika Kusini na Ulaya Mashariki walipitia angalau aina moja ya unyanyasaji wa kingono au unyonyaji kwenye majukwaa ya mtandaoni mwaka mmoja kabla ya utafiti huu kufanyika.

Ripoti imebaini kuwa takriban watoto milioni 15 katika nchi zilizofanyiwa utafiti waliwekwa wazi kwa maudhui ya ngono bila kupenda, milioni 9 walishinikizwa katika mazungumzo ya ngono au kushiriki picha za ngono, na milioni 4 walishiriki picha za ngono bila idhini yao.

Utafiti huo, ambao UNICEF iliuelezea kama moja ya tafiti kubwa zaidi za aina yake, ulitokana na tafiti za kitaifa zilizokusanywa kati ya mwaka 2020 na 2025 za watoto wapatao 21,000 wanaotumia mtandao katika nchi 21, ambazo ni pamoja na Kenya, Pakistan, Brazil na Serbia.

Aidha ripoti imegundua kuwa, karibu asilimia 60 ya unyanyasaji ulioripotiwa ulitokea kwenye mitandao ya kijamii, ikiongozwa na Facebook, WhatsApp, Instagram, Snapchat na TikTok, huku asilimia 14 ikitokea kwenye michezo ya mtandaoni.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii