Rais Vladmir Putin amesema bado kuna nafasi ya kufikiwa kwa makubaliano ya amani Ukraine, huku akielezea maonyo ya Ukraine kuhusu hatari kwa ndege zinazotumia anga ya Urusi kuwa sawa na ugaidi unaofanywa na serikali.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema bado kunayo nafasi ya kupatikana kwa makubaliano ya amani yatakayomaliza vita vya Ukraine. Akizungumza katika mkutano wa kiuchumi mashariki mwa Urusi, Putin amesema mataifa kadhaa, yakiwemo Marekani na China, yako tayari kuunga mkono juhudi za kusaka suluhisho la amani.
Rais huyo wa Urusi hata hivyo amesema suluhisho la kudumu linapaswa kupatikana kupitia mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine, ambazo ndizo pande zinazohusika moja kwa moja katika mzozo huo.
Putin ametoa kauli hizo wakati mashambulizi yakiendelea kushuhudiwa kati ya pande hizo mbili. Katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo, mtu mmoja ameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa katika shambulio la droni lililolenga basi la abiria katika mkoa wa Belgorod nchini Urusi. Mamlaka za eneo hilo zimesema shambulio hilo lilmetokea, karibu na mpaka wa Ukraine.