Zambia ilizifunga shughuli za mahakama zote nchini hapo jana kwa kile ilichokiita sababu za kiusalama, hatua iliyozua ukosoaji mkali kutoka kwa wanasheria na makundi ya kutetea haki za binaadamu.
Hatua hiyo ilikuja siku ya mwisho ya kisheria ya kuwasilisha pingamizi dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 13, ambapo Rais Hakainde Hichilema alitangazwa mshindi wa muhula wa pili kwa kupata takriban asilimia 60 ya kura.
Kiongozi wa upinzani, Brian Mundubile, alikuwa ametangaza nia ya kupinga matokeo hayo mahakamani, lakini amejificha baada ya watu 11 wa karibu naye kukamatwa kwa madai yanayohusiana na uhaini. Wakati wa operesheni hiyo, aliyekuwa waziri wa serikali iliyopita, Mutotwe Kafwaya, aliuawa kwa kupigwa risasi.
Mashirika ya kiraia na Chama cha Wanasheria Zambia yamesema kufungwa kwa mahakama kunahatarisha haki ya wananchi kupinga matokeo ya uchaguzi na kunatilia shaka uwazi wa mchakato wa kidemokrasia nchini humo.