Makamu wa Rais wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kuanzia Septemba 4, 2026, chini ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika barua ya Agosti 25, 2026 iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Nchimbi amesema amemwandikia Rais Samia kumjulisha kuwa ameamua pia kustaafu siasa na utumishi wa umma.
Nchimbi amesema uamuzi wake umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 50(2)(c), ikisomwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba ya Tanzania. Ibara hizo zinaweka mazingira na utaratibu wa mwenye dhamana ya kikatiba kujiuzulu.
Lakini sehemu inayovuta zaidi hisia katika barua hiyo ni maelezo yake kuhusu ahadi aliyompa Rais Samia Agosti 27, 2025—kwamba angemtumikia kwa uwezo na uaminifu, lakini angeachia nafasi iwapo Rais angehitaji Makamu mwingine.