Aliyetimuliwa Man Utd Kuwa Kocha Mpya AC Milan ya Italia

Kocha raia wa Ureno, Ruben Amorim, anatarajiwa kuwa kocha mkuu mpya wa klabu ya Italia, AC Milan, baada ya kukubaliana kwa masharti ya awali kujiunga na timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Italia, Amorim bado hajatia saini rasmi mkataba huo, lakini inasemekana atawasili Milan baadaye wiki hii ili kukamilisha dili la miaka miwili kuchukua mikoba ya Massimiliano Allegri, ambaye alifutwa kazi kufuatia matokeo mabaya yaliyoifanya klabu kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ripoti zinaeleza kuwa Amorim amekubali kuachana na malipo yaliyosalia kutoka kwa klabu ya Manchester United baada ya kuondolewa kwake Januari, hatua inayotajwa kuonyesha nia yake ya kuanza ukurasa mpya wa kazi yake ya ukocha.

Amorim, ambaye alijijengea jina kubwa akiwa Sporting Lisbon kwa kuipatia ubingwa wa ligi baada ya miaka 19, anarejea Ulaya akiwa mmoja wa makocha vijana wanaoheshimika zaidi kutokana na mbinu zake za kisasa za uchezaji.

Iwapo dili hilo litakamilika kama ilivyotarajiwa, mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa AC Milan utakuwa mechi ya kirafiki dhidi ya Celtic tarehe 25 Julai, kabla ya kumaliza maandalizi ya msimu kwa mchezo dhidi ya Manchester United tarehe 15 Agosti.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii